January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabati yasiyokidhi viwango yaingizwa na kusambazwa

Mabati yakiwa sokoni tayari kwa kuuzwa

Mabati yakiwa sokoni tayari kwa kuuzwa

Spread the love

SERIKALI imeshidwa kuwajibika katika kuzuia kasi ya uingizwaji nchini wa bidhaa sizokidhi viwango vya ubora. Anaandika Pendo Omary .… (endelea).

Kutokana na uzembe huo, kampuni ya Uni Metal East Africa Limited imethibitishwa kuingiza nchini na kusambaza mabati yasiyokidhi viwango vya ubora tani 15,000.

Sababu kubwa inayotajwa kuchochea msururu wa bidhaa hizo nchini ni kuwepo kwa mfumo mbovu katika kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa.

David Kafulila- Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), amefichua udhaifu huo wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Amesema mabati hayo yaligundulika baada ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kufanya ukaguzi katika ghala linalotumika kuhifadhi mabati ya kampuni hiyo 14 Aprili mwaka huu.

Kafulila ambaye pia ni msemaji mkuu wa kambi ya upinzani bungeni kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, amesema mabati hayo yanazalishwa na kampuni ya Manaksia Limited iliyopo nchini ndia.

“Aidha, 19 Februari mwaka huu, Dk. Abdallah Kigoda – Waziri wa Viwanda na Biashara alitoa tamko akiitaka Uni Metal East Africa Limited kutoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari kuhusu kusambaza mabati feki, kisha mabati hayo yakusanywe na kuteketezwa,”amesema Kafulila.

Uni Metal East Africa limited ilitoa tangazo kwa umma Machi 26 mwaka huu, ikiwa ni siku 35 au wiki 5 baada ya tangazo la waziri.

“Hawa wafanyabiashara ni jeuri. Ni kwa sababu wameiweka mfukoni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ). TRA ni kichaka cha kuingiza bidhaa feki. Imejaa rushwa, ” anadai Kafulila.

Kafulila amesema, mbali na rushwa iliyotawala TRA, kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo ni takribani kilometa 70. Kwamba “…katika eneo hili kuna bandari bubu zaidi ya 30. Polisi wanajua. Wanahangaika na madereva wa bodaboda. Wameshidwa kuzidhibiti.”

“Watu walionunua mabati wameumia. Ujenzi umeathirika. Serikali ichome mabati yote yaliyopatikana,” ameomgeza Kafulila.

Akizungumza na MwanaHALISIOnline, Bitaho Baptister – mwanasheria wa TBS amesema, “Adhabu ya kwanza ni kutekeleza agizo la waziri. Akishidwa, Sheria ya Viwango namba mbili ya mwaka 2009 kifungu cha 27 anaadhibiwa kwa kutoa faini ya milioni 50 au miaka miwili jela au vyote kwa pamoja na kufutiwa  lesi ya viwango na ubora”.

Amesema, muda wowote TBS itafanya ukaguzi wa kushtukiza katika ghala za Uni Metal East Africa Limited kuangalia kama bado wameficha mabati mengine feki, kisha kuyachoma yale yaliyopatikana baada ya kukusanywa.

Baptister amesema, “TBS ina changamoto ya uhaba wa watendaji ambapo waliopo sasa ni 230 nchi nzima. Mara kadhaa wameiomba serikali kuongeza watendaji bila mafanikio.”

MwanaHALISIOnline imezungumza na waziri Kigoda kwa njia ya simu kuhusu hatua ya utekelezaji wa agizo lake. Amesema “ Hili suala bado tunalifanyia kazi kwa karibu.”

Pia MwanaHALISIOnline limefika katika ofisi za Uni Metal East Africa Limited zilizopo eneo la Tazara jijini Dar es Slaam, ili kujua ni kwa nini agizo la waziri Kigoda limechelewa kutekelezwa.

Meneja Utawala wa kampuni hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake amesema “I can’t talk anything” (siwezi kuzungumza chochote).

error: Content is protected !!