WAZIRI Ofisi ya Rais-Tamisemi nchini Tanzania, Ummy Mwalimu, amepiga marufuku kitendo cha vikao vya mabaraza ya madiwani, kufanyika bila ya uwepo wa wabunge wa maeneo husika. Anaripoti Noela Shila, TUDARCo … (endelea).
Waziri Ummy ametoa marufuku hiyo leo Ijumaa, tarehe 20 Agosti 2021, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.
“Kwa hiyo narudia kuelekeza vikao vya mabaraza ya madiwani vifanyike wakati Bunge halipo, ili kuwapa fursa wabunge kuhoji na kufuatilia matumizi ya hizi fedha,” amesema Waziri Ummy.
Waziri huyo wa Tamisemi, amesema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri, kuandaa vikao vya mabaraza hayo, wakati wabunge wa maeneo yao hawapo.
“Changamoto kubwa inayotokea mara nyingi, unakuta wakurugenzi na madiwani wanasubiri wabunge wakiwa hawapo, wao ndiyo wanafanya vikao vya mabaraza ya madiwani,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy, ameyaagiza mabaraza ya madiwani na wabunge, kubeba jukumu la kusimamia utekelezwaji wa miradi ya maendeleo iliyoko kwenye maeneo yao, ili kudhibiti vitendo vya ubadhirifu wa fedha.
“Tunayo mabaraza ya madiwani na mimi nirudishe kazi hii kwa mabaraza, wao ndiyo wako pale kwenye halmashauri kuhakikisha hizi pesa tulizopeleka zinatumika vizuri,” amesema Waziri Ummy na kuongeza:
“Wajibu wa madiwani husika katika halmashauri husika, ni kuhakikisha fedha zinafanya kazi iliyokusudiwa, tunao wabunge ambao wamekuwa wasimamizi wazuri wa utekelezaji miradi, waendelee kufanya kazi hiyo.”
Leave a comment