May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabadiliko Yanga, Kikwete awapa ujumbe

Spread the love

 

RAIS mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa Klabu ya Yanga kuwa wawazi kushauri na kukosoa ili iweze kusonga mbele. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Kikwete amesema hayo leo Jumapili, tarehe 27 Juni 2021, katika mkutano mkuu wa Yanga, uliofanyika ukumbi wa DYCCC-Temeke, mkoani Dar es Salaam.

Lengo la mkutano huo ni kufanya mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo ili kuiwezesha kuanzia kuendeshwa kisasa.

Kikwete aliyekuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 ambaye ni shabiki wa Yanga amesema, alipopelekewa mwaliko na mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk. Mshindo Msolla, hakusita kwani agenda zake zilimvutia.

 

Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete

“Niwaombe wana Yanga wenzangu, mzitumie vizuri fursa mnazopewa kwa kutoa maoni na ushauri unaojenga ili kuitoa Yanga hapa na kuipeleka mbele.”

“Kwenye upungufu mnasema, kwenye mazuri mnasema na kwenye kukosoa unakosoa ila kosoa ili mambo kesho yawe mazuri, usikosoea kwa kumoa unakuwa unashiriki kubomoa,” amesema Kikwete huku akishangiliwa.

“Msiache kusema kwenye mikutano kama hii, mnaenda kunung’unika vijiweni, huo ni useng’enganji, uchimvi ni mambo ambayo hayasaidii kujenga, yanaleta mpasuko usiokuwa na tija klabuni na watu wa aina hii msiwaendekeze, waambieni,” amesema.

Amesema, mabadiliko hayo ni shirikishi kwa kuitaka wanachama na kutoa elimu ya jinsi yanavyokwenda hivyo, wamewataka kushirikiana kwani mabadiko kama hayo yanafanyika hata serikalini.

“Jambo usipolieleza vizuri likaeleweka, wanaweza kulikataa, kwa hiyo Dk. Msolla umefanya vizuri sana kwa kuwashirikisha mpaka sasa kilipofikia hatua ya maelewano ya waliowengi,” amesema.

Dk. Mshindo Msolla, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga

Kikwete amesema, mabadiliko ni lazima “na kila kitu kinakwenda na wakati huo, wakati tulionao sasa si wakuendesha klabu kama zamani, lakini lazima mtengeneza mambo ambayo mtatoka hapa kwenda mbele na ndiyo mtaishi kauli ile ya daima mbele, nyuma mwiko.”

Akihitimisha hotuba yake, Kikwete amesema “Yanga naipenda, inapofanya vizuri nafurahi sana na inapofanya vibaya nasononeka na matumaini yangu Jumamosi ijayo itafanya vizuri.”

Yanga itacheza na Simba, mchezo wa ligi kuu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 11 jioni ya tarehe 3 Julai 2021.

error: Content is protected !!