Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mabadiliko ya sheria ya usalama wa taifa yazua mjadala
Habari za SiasaTangulizi

Mabadiliko ya sheria ya usalama wa taifa yazua mjadala

Kiongozi wa Kanisa la Uamsho la Moravian, Askofu Emmaus Mwamakula
Spread the love

 

SERIKALI iko mbioni, kuwasilisha bungeni muswaada wa marekebisho ya sheria ya Idara ya Usalama wa taifa (TISS), uliosheheni utata, ikiwamo kuweka kinga dhidi ya maofisa wa idara hiyo, kutofikishwa mahakamani wanapotenda kazi zao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka Dodoma zinasema, muswaada huo, unatarajiwa kufikishwa bungeni katika mkutano huu wa Bunge la bajeti, unaotarajiwa kufikia mwisho wake, Julai mwaka huu.

Miongoni mwa vifungu vinavyolenga kufanyiwa marekebisho, ni kifungu cha 19 kinachopendekeza kuweka kinga dhidi ya makosa ya jinai kwa maafisa wa idara hiyo, pale wanapokuwa wanatimiza majukumu yao.

Sheria ya sasa ya usalama wa taifa, iliyotungwa mwaka 1996 wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa, kinga ilitolewa katika mashauri ya madai pekee dhidi ya maafisa hao.

Colonel Apson Mwang’onda, ndiye aliyekuwa mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa nchini, wakati sheria ya kwanza ya idara hiyo, ilikuwa ikitungwa.

Apson alifariki dunia, tarehe 7 Oktoba 2019, kwa ugonjwa wa saratani, nchini Afrika Kusini, alikokuwa amekwenda kwa matibabu. Alikuwa na miaka 75 na akiwa tayari amestaafu utumishi wa umma.

“Kwamba, muswaada ukiwa sheria, afisa wa usalama wa taifa, atakuwa juu ya sheria nyingine za nchi zinazozuia makosa ya jinai, kutokana na kulindwa na sheria hiyo,” anaeleza kada mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Naye Kiongozi wa upinzani nchini, Tundu Lissu amesema, “mapendekezo haya yakipitishwa na Bunge na kuwa sheria, itaweza kuibua mgogoro wa kikatiba, kutokana na Katiba ya Jamhuri inayoelekeza kuwa watu ni sawa mbele ya sheria.”

Aidha, mabadiliko ya sasa yanalenga kuiondoa idara kutoka usimamizi wa waziri mwenye dhamana na masuala ya usalama wa taifa na kulikabidhi jukumu hilo moja kwa moja kwa rais.

Mapendekezo mengine yaliyomo kwenye muswada, ni pamoja na vifungu vya 11, 15, 18, 19 (3) vinavyoondoa mamlaka ya usimamizi kwa waziri wa mambo ya nje, katibu mkuu kiongozi na mwanasheria mkuu wa serikali, katika masuala mbalimbali yanayohusu “usimamizi wa intelijensia na usalama.”

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Kwa upande wake, Askofu Mkuu Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki, Emmaus Bandekile Mwamakula, anaeleza kuwa muswaada huo, haupaswi siyo kujadiliwa na Bunge, bali hata kufikishwa mbele ya wabunge.

“Kwa mtazamo wetu sisi Askofu Mwamakula, muswada huu unalenga sana kukuza vitendo vya utekaji na uuaji nchini. Badala ya kuwekeza zaidi katika kutoa mafunzo ya ueledi na uadilifu kwa maafisa wa usalama, serikali inawewekea kinga ili wasiwajibike kwa uzembe, uuaji na utekaji uliofanywa kwa makusudi na ubinafsi wao na viongozi,” ameeleza.

Anasema, “muswada huu ukipita, utahalalisha vitendo vya utekaji, upotezwaji na hata mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kwani viongozi watatumia mwanya huo kunyamazisha watu wasiowataka katika jamii.

“Muswada unataka sisi sote tuamini kwamba viongozi wa serikali yetu, wote ni malaika na hawataweza kuitumia vibaya kinga hiyo ili kuwamaliza wapinzani wao.”

Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene

Askofu Mwamakula anasema, muswada huo unakuja katika kipindi ambacho kuna kelele kubwa sana katika jamii kutaka ufanyike uchunguzi ili kuwabaini watu waliofanya mauaji na unyama katika kipindi cha utawala wa John Magufuli.

“Hili ni jambo la kushangaza sana. Kwamba serikali inapeleka muswaada bungeni kulinda ukatili uliofanywa katika utawala wa Awamu ya Tano? Hapana! Hili ni jambo la kushangaza sana,” anaeleza.

Katika andishi lake alilolisambaza kupitia mitandao ya kijamii, Askofu Mwamakula anahoji: “Serikali inalenga nini kwa kupeleka muswada huo bungeni kwa sasa? Inataka kumkinga nani ili asichunguzwe kwa mauaji na utekaji ambao ulifanyika nchini katika miaka ya hivi karibuni? Viongozi wetu wanahofia nini?”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!