October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabadiliko ya sheria inayowahusu mawakili wasomwa bungeni

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania, imewasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2020 bungeni ambao pamoja na mambo mengine, unapendekeza mawakili wanaoteuliwa katika nafasi za uandamizi kwenye utumishi wa umma, wasifanye kazi za uwakili wa kujitegemea wakiwa kwenye nafasi zao. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Hayo yamesemwa leo Jumatatu bungeni jijini Dodoma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa  Adelardus Kilangi wakati akiwasilisha maelezo ya muswada huo unaopendekeza kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali 14.

Amesema, muswada huo umegawanyika katika sehemu 15. Sehemu ya kwanza inaweka masharti ya awali ikijumuisha jina la muswada na masuala ya utangulizi.

Baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye muswada huo, Profesa Kilangi amesema, sehemu ya pili ya muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya  Mawakili Sura ya 341, kwa kuongeza Kifungu kipya cha 3A ili kuondoa uwezekano wa mgongano wa maslahi unaoweza kujitokeza kwa mawakili  anaoteuliwa katika nafasi za uandamizi katika Utumishi wa Umma.

“Hivyo, inapendekezwa kuwa wanaoteuliwa wasifanye kazi za uwakili wa kujitegemea wakiwa katika nafasi hizo,” amesema Profesa Kilangi.

“Aidha, inapendekezwa, katika kipindi chote cha utumishi wao, viongozi hao pamoja na mawakili wote wa Serikali wasilipe ada za uanachama za kila mwaka na malipo mengine yanayolipwa na mawakili chini ya Sheria hii kwa kuwa katika kipindi hicho chote hawatakuwa wanajishughulisha na kazi za uwakili wa kujitegemea,” amesema.

AG huyo amesema sehemu ya tatu ya muswada unapendekeza kurekebisha Sheria ya Mfuko wa Pembejeo, Sura ya 401 ambapo katika kifungu cha 2, inapendekezwa kuongeza tafsiri ya msamiati “Agricultural machinery” ndani ya sheria hiyo kwa lengo la kutoa tafsiri pana ya msamiati huo kujumuisha nyenzo zote muhimu zilizokusudiwa na Sheria.

Amesema, Kifungu cha 7 kinarekebishwa ili kuainisha wajumbe wa Bodi ya Wadhamini watakaoteuliwa na Waziri.

Amesema, kwa sasa kifungu hiki kinampa mamlaka waziri kuteua wajumbe wa Bodi wasiopungua sita na wasiozidi 10 bila kubainisha wasifu na sehemu wanakotoka wajumbe hao.

“Lengo la marekebisho haya ni kuhakikisha kuwa Bodi inakuwa na uwakilishi stahiki ili kuwezesha na kuboresha utekelezaji wa majukumu yake,” amesema.

Profesa Kilangi amesema, inapendekezwa kuwa, kifungu kipya cha 9A kiongezwe ili kuweka utaratibu wa kuomba mikopo katika Mfuko wa Pembejeo.

Amesema, hali kadhalika, kifungu kipya cha 12A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka utaratibu wa rufaa kwa mtu asiyeridhika na maamuzi ya Bodi.

Amesema, lengo la marekebisho haya ni kuweka mfumo madhubuti wa kushughulikia malalamiko ya wadau dhidi ya Mfuko wa Pembejeo.

Hata hivyo, Salome Makamba, msemaji mkuu wa kambi rasmi wa wizara ya katiba na sheria amesema, ukiangalia mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, utagundua kwamba si vifungu vyote vinavyofanyiwa mapendekezo na au vifungu vilivyokuwepo katika sheria mama ambavyo vinaondoa kero ya wakulima kwenye pembejeo

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza, mabadiliko kwenye sheria hii, iongeze kifungu cha kuitaka serikali kuhakikisha inatenga asilimia 40 ya bajeti ya wizara ya kilimo kwa ajili ya pembejeo za kilimo,” amesema Salome ambaye pia ni mbunge wa viti maalum (Chadema).

Amesema, aidha ni muda sasa kupitia marekebisho ya sheria hii kuongeza kifungu kinachotoa adhabu kali kwa watumishi wa Serikali wanaotumia madaraka yao vibaya na kuiba pembejeo ambazo zinalenga kuwasaidia wakulima na badala yake zinaishia kuwanufaisha watendaji wa serikali huku wakulima wakikosa pembejeo.

Katika sehemu ya nne ya muswada huo, Profesa Kilangi amesema, inapendekeza marekebisho katika Sheria ya Umeme, Sura ya 131, ambapo katika kifungu cha 3 tafsiri ya misamiati “licensee” na “supply” inarekebishwa kwa lengo la kuboresha tafsiri ya misamiati hiyo na pia kuongeza tafsiri ya misamiati mingine ambayo kwa sasa haijatafsiriwa katika Sheria.

Amesema, Kifungu kipya cha 4A kinapendekezwa kuongezwa ili kuainisha nafasi ya Kamishna wa Masuala ya Umeme na kuainisha mamlaka na majukumu yake.

“Lengo la marekebisho haya ni kutambua kisheria nafasi na majukumu ya Kamishna wa Masuala ya Umeme kama ilivyo kwa makamishna wengine wa mafuta na madini na ambao nafasi na majukumu yao yametambuliwa kwenye sheria za tasinia zao,” amesema.

Amesema, Kifungu cha 6 kinarekebishwa ili kuiondolea EWURA jukumu la kushughulikia upatikanaji wa ardhi kwa kuwa zipo mamlaka zenye jukumu hilo kisheria.

“Inapendekezwa pia kuainisha ukomo wa muda ambao mtu atapaswa kukata rufaa kwenye Baraza Huru la Ushindani,” amesema

“Kifungu kipya cha 14A kinapendekezwa kuongezwa kwa lengo la kumpa wajibu mtoa huduma kuondoa mitambo na miundombinu ya umeme baada ya muda wa mkataba kuisha,” amesema

error: Content is protected !!