October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mabadiliko tabianchi yabadili mvua za masika, TMA yatoa mapendekezo 5

Spread the love

 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema, mvua za masika Machi- Mei mwaka 2022 zinatarajiwa kuwa chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi nchini kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mabadiliko hayo yanaweza kuathiri sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile usafirishaji, afya, nishati, madini na shughuli za kilimo.

Katika msimu wa masika 2022, kubadilika kwa joto la bahari kwa muda mfupi kulikojitokeza kipindi cha mwezi mmoja ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, tarehe 13 Aprili 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam, kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari katika mwenendo wa hali ya hewa wakati wa mvua za masika.

Amesema, hali hiyo imesababisha kuvurugika kwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kuathiri unyeshaji wa mvua za masika nchini Tanzania na katika eneo la pembe ya Afrika na ukanda wa Afrika Mashariki.

Amesema maeneo tarajiwa yatakayoathirika ni ya Pwani ya Kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga.

Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa ukanda wa Ziwa Victoria mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.

Dk. Kijazi amezitaja athari zinazotarajiwa ni upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo ambapo hali hii inaweza kuathiri ukuaji wa mazao, upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini.

“Upo uwezekano wa kuongezeka kwa athari za magonjwa ya kuambukizwa hususan magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama kwa afya,” amesema

Ametaja athari zingine ni vipindi virefu vya ukavu, milipuko ya wadudu-dhurifu kwa mazao kunaweza kusababisha athari za kunyauka kwa mimea.
Amesema, shughuli za ujenzi, usafiri na usafirishaji zinatarajiwa kunufaika katika vipindi vya mvua chache.

Dk. Kijazi amesema, kutokana na hali hiyo hatua za kuhifadhi maji zinahitajika ili kuvuna maji wakati wa vipindi vya mvua kwa lengo la kuondoa upungufu wa maji unaoweza kujitokeza.
Ametumia fursa hiyo kutoa mapendekezo matano.

Mosi, wakulima washauriwe kuzingatia matumizi ya mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kihifadhi maji na unyevunyevu wa udongo.

Pili, elimu kwa jamii itolewe ili kuweka mpango mzuri wa matumizi endelevu ya rasilimali za maji na uhifadhi wa malisho.

Tatu, wizara na mamlaka husika zishauriwe kushirikiana na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula, malisho ya mifugo, maji na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na hali ya upungufu wa mvua uliopo na uwezekano wa mvua chache zinazotarajiwa.

Nne, kutekeleza mikakati ya ushirikiano na sekta binafsi katika kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha ili kuimarisha uwekezaji na kulinda mitaji ya kibiashara.

Tano, kuimarisha mifumo ya mawasiliano na mrejesho katika kusambaza taarifa za hali ya hewa, kuendelea kuboresha miundombinu ya hali ya hewa na mifumo ya mawasiliano ili jamii ipate taarifa za hali ya hewa kwa wakati na kuzitumia

error: Content is protected !!