Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Maaskofu Katoliki Tanzania watoa waraka wa Kwaresima, wagusia upatanisho
Habari MchanganyikoTangulizi

Maaskofu Katoliki Tanzania watoa waraka wa Kwaresima, wagusia upatanisho

Rais wa TEC, Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga
Spread the love

 

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetoa waraka wa Kwaresima wa mwaka 2022 ambao kwa sehemu kubwa umejikita kuzungumzia umuhimu wa upatanisho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Waraka huo wenye kurasa 44, umetolewa na maaskofu hao katoliki 35 ikiwa leo ni mwanzo wa kipindi cha Kwaresima ‘Jumatano ya Majivu’ tarehe 2 Machi 2022.

Waraka huo, umebeba ujumbe unaosema “Tunawasihi kwa jina lake Kristo, Mpatanishwe na Mungu” (2 Kor 5:20).

Katika sura hii, Mtume Paulo ametoa maelezo mbalimbali kumhusu Kristo na mwishoni anahitimisha na kumsihi kila mmoja ajitahidi kupatanishwa na Mungu.

Mwaliko huu ni kiashirio kwamba, maisha ya mkristo lazima yaambatane na jitihada ya kutaka kupatanishwa na Baba wa mbinguni kwa sababu baada ya maisha haya tutarudi kwake.

“Mafundisho yote yanayohusu upatanisho ni kipengele muhimu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Upatanisho ni neno ambalo mwanadamu hukutana nalo mara nyingi asomapo Maandiko Matakatifu na ndani ya jamii anamoishi. Upatanisho ni sehemu ya wokovu wetu; unakuza mahusiano yetu na Mungu na pia kati yetu,” unaeleza waraka huo

Kisiasa, maaskofu hao wakiongozwa na Gervas Nyaisonga, Askofu Mkuu ambaye pia ni Rais wa Baraza hilo wanasema, upatanisho husaidia watu kuwa huru, kuwajibika, kwa kutetea haki zao na za wengine; kushiriki katika ujenzi wa Taifa kwa umoja, juhudi na maarifa; na kujenga demokrasia kwa kushiriki katika chaguzi zilizo huru na za haki.

Wanasema, mchakato wa upatanisho husaidia watu kuishi kwa umoja na amani. Lakini uovu hauwezi kuisha maadamu tunaishi katika ulimwengu huu uliogubikwa mafarakano; na upatanisho wa kweli ni tumaini la binadamu yeyote anayemwogopa Mungu.

Dunia inahitaji kwanza kupatanishwa na Mungu na kisha upatanisho ndani ya jamii. Pasiwepo watu ambao maisha yao yote ni ya manung’uniko sababu tu njia za upatanisho zimefungwa na upande wa pili. Sote tunaalikwa ndani ya jamii ya kitanzania kulitazama na kulifanyia kazi hilo katika ukweli na uadilifu.

“Kisiasa, ‘upatanisho’ wa kweli hupatikana katika kuitafuta, kuiishi na kuilinda demokrasia na amani dumifu,” unaeleza waraka huo na kuongeza:

“Ili kufikia demokrasia ya kweli kama njia ya kuelekea mapatano ya kweli, bado yanahitajika majadiliano kati ya wadau mbalimbali wa kisiasa na hasa katika vikao muhimu vya kutoa uamuzi.”

“Hivyo basi, viongozi wetu hawana budi kubadilika kuona kwamba demokrasia na utawala bora vinashika hatamu kwa ajili ya manufaa ya wengi.”

Baadhi ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania

Maaskofu hao wanasema, “wakati huu wa Kwaresima, kila mmoja katika Taifa la Mungu anahimizwa kutekeleza wajibu wake, kwa njia ya toba, kujenga na kudumisha moyo wa mapatano na uelewano katika jamii.”

“Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa aina yoyote ile, hususan ubaguzi wa kisiasa. Wakristo hawana budi kuwa ni wadau wa amani ili kudumisha mapatano ya kweli. Haya yote yatawezekana iwapo tu haki, amani, ukweli na uwazi vitatamalaki,” wamesisitiza

Waraka huo unahitimishwa ukisema, “ujumbe huu wa Kwaresima kwetu ni mahususi kwa ajili ya ujenzi wa jamii mpya yenye nia ya kuishi kwa umoja na amani kama asemavyo Mzaburi “Tazama, jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, ndugu wakae pamoja kwa umoja” (Zab 133:1).

“Kukaa huku pamoja haimaanishi kwamba ni kukaa bila tofauti za kimawazo na kimtazamo. La hasha. Bali ni kule kukaa kwa kukubali tofauti hizo bila ya kufarakana,” wanasema

Maaskofu hao wanasema, yumewaandikia ujumbe huu wa Kwaresima kwa Mwaka 2022: “Tunawasihi kwa jina lake Kristo, mpatanishwe na Mungu” (2 Kor 5:20), tukitambua kwamba hapa na pale jamii zetu zinafarakana kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kimtazamo.

“Ndiyo maana tumesisitiza na tunasisitiza kwamba hayo yanapotokea tunahitaji kupatanishwa. Lengo kuu la upatanisho si kuonekana kwamba mmoja ameshindwa bali ni “kuanza maisha mapya; maisha ya neema.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

GGML kuwapatia mafunzo kazi wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini

Spread the loveJUMLA ya wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini wamepata fursa...

Habari Mchanganyiko

NHC yaongeza mapato kufikia kufikia Sh bilioni 257

Spread the loveSHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeongeza mapato hadi kufikia...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mo Dewji achomoza bilionea pekee Afrika Mashariki

Spread the loveMAZINGIRA mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania yamezidi kuleta matunda baada...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia: Panapotokea uvunjifu wa amani panakuwa haki imepotezwa

Spread the love  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu...

error: Content is protected !!