July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maandamano wakulima Mbeya yanukia

Spread the love

 

WAKULIMA mkoani Mbeya wanakusudia kufanya maandamano muda wowote katika siku ya leo au kesho ili kuishinikiza serikali kutengua amri yake ya kuwataka wakulima hao kutofunga bidhaa za kwa mtindo wa ‘lumbesa’, anaandika Charles William.

Amri ya kuwataka wakulima kutofunga mazao yao katika gunia linalozidi 100 kilogramu ilitolewa hivi karibuni na Majaliwa Kassim, Waziri Mkuu wa Tanzania na kuagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia agizo hilo.

Amri hiyo ya serikali imepelekea magunia ya wakulima wa viazi mviringo wilayani Rungwe, Mbeya kuanza kukamatwa na kutozwa faini kwa kila mzigo unaozidi 100 Kg. jambo ambalo limezua malalamiko na tishio la maandamano.

“Walitaka kuandamana toka juzi, tukawatuliza lakini sidhani kama wanaweza kutulia tena kwasababu uonevu wanaofanyiwa hauvumiliki na wanaweza kuandamana muda wowote,” ameeleza Friday Joseph Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndaza, kata ya Ndato wilayani Rungwe.

Kijiji hicho ni miongoni mwa maeneo ambalo magari mengi ya magunia ya viazi yamerejeshwa ili kufumuliwa na kufungwa upya baada ya kutozwa faini.

“Serikali imeagiza wafunge mizigo isiyozidi 100 Kg. lakini hakuna mifuko inayotosha uzito huo, mifuko iliyopo mingi inazidi kwahiyo wanakadiria uzito na ukizidi wanakamatwa Uyole na kutozwa faini ya Sh. 10,000/=,” ameeleza zaidi.

Wakulima hao ambao soko lao kubwa la viazi mviringo ni Dar es salaam wamelalamikia serikali kuwakataza wao kufunga mizigo inayozidi 100 kg. na kuwatoza faini kubwa huku magunia kutoka mikoa mingine yakiendelea kufungwa kwa mtindo la ‘lumbesa’ hali inayofanya magunia kutoka Mbeya yasinunuliwe.

“Kama tunalima wenyewe kwa gharama zetu, inakuwaje serikali inakuja kutupangia ukubwa wa mzigo tunaouza? Kama wanataka tusizidishe hata kilo moja kwanini hawaji tuwauzie wao hivyo viazi? Mbona hawajawahi kuja kusimamia bei ya mbolea tunayonunua?” amehoji kwa hasira John Mwamanda mmoja kati ya wakulima.

Mwanahalisi online imemtafuta pasipo mafanikio Amos Makala Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ili kuzungumzia sakata hilo ikiwemo Serikali mkoani humo kukamata magunia ya wakulima hao na kuyatoza faini huku ikiamuru kurudishwa shambani kwaajili ya kufumuliwa.

Licha ya kupigiwa zaidi ya mara tano kwa nyakati tofauti tofauti Mkuu huyo wa Mkoa simu hiyo ilikuwa ikikatwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi hakuweza kujibu.

Akitoa maoni yake juu ya hali inayoendelea juu ya sakata hilo, John David Fungo Mkazi wa kata ya Ndato wilayani Rungwe ambapo ndipo yalipo mashamba mengi ya wakulima wa viazi, ameitaka serikali kutumia busara ili kutoendelea kuwaumiza wakulima na kuepusha maandamano.

“Uzito wa viazi unatofautiana, wakulima wanafunga viazi katika gunia lakini wakifika kwenye mzani wanaambiwa kilo zimezidi wanatozwa faini wakati huohuo hata hiyo mifuko ya kilo 100 haipatikani watu wanakadiria tu,

Kuna baadhi ya maeneo magunia ya ‘lumbesa’ hayazuiliwi kwahiyo magunia ya wakulima hawa ndiyo yanayokosa wateja sokoni kwa kuonekana madogo hivyo kuwatia hasara wakulima hawa ambao wanalima kwa gharama kubwa na wanategemea kilimo hiki kuendesha maisha yao,” Ameeleza.

error: Content is protected !!