WAZIRI Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok, aliyewekwa madarakani na jeshi la nchi hiyo Novemba 2021, amejiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi, wanaoshinikiza utawala kisiasa na kiraia. Unaripoti Mtandao wa BBC Swahili … (endelea).
Hamdok alitangaza hatua hiyo jana Jumapili, tarehe 2 Januari 2022, baada ya kuibuka maandamano ya wananchi wanaopinga makubaliano kati ya Waziri Mkuu huyo na Jeshi la Sudan. Watu wawili wamepoteza maisha katika maandamano hayo.
Akihutubia wananchi kupitia Televisheni ya Taifa ya Sudan, Hamdok alisema amejiuzulu, ili kuinusuru nchi hiyo iliyokuwa katika kipindi cha hatari kinachotishia ustawi wake.
“Niliamua kurudisha jukumu hilo na kutangaza kujiuzulu uwaziri mkuu, na kutoa nafasi kwa mwanaume au mwanamke mwingine wa nchi hii adhimu, ili kuisaidia kupita kile kilichosalia cha kipindi cha mpito kwa nchi kuelekea utawala wa kidemokrasia ya kiraia,” alisema Hamdok.
Wananchi wa Sudan wanapinga makubaliano ya Jeshi la nchi hiyo na Hamdok, ya kugawana madaraka na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa mapinduzi yaliyonng’oa madarakani aliyekuwa Rais wao, Omar al Bashir.
al Bashir aling’olewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi 2019, kisha Serikali ya Mpito iliundwa na Jeshi, iliyodumu kwa muda mfupi baada ya wananchi kuandamana wakishinikiza upatikanaji wa Serikali ya kidemokrasia.
Kufuatia maandamano hayo, Hamdok aliwekwa madarakani kwa ajili ya kuongoza Serikali ya mpito hadi 2023, Taifa hilo litakapofanya uchaguzi wa kuunda Serikali ya kiraia.
Leave a comment