SERIKALI ya Tanzania imesema maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19), katika kipindi cha tarehe 29 Oktoba hadi 2 Desemba 2022, yameongezeka kwa asilimia 62.5, kutoka visa vipya 272 hadi kufikia 442. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa jana Jumatatu, tarehe 6 Desemba 2022 na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu, akitoa mwenendo wa UVIKO-19 nchini.
“Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya UVIKO-19 nchini na inaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu. Katika kipindi cha tarehe 29 Oktoba hadi 2 Desemba 2022, jumla ya visa vipya 442 vimethibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO-19. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na takwimu za mwezi ulipita ambapo kulikuwa na visa 272 sawa na ongezeko la asilimia 62.5,” imesema taarifa ya Prof. Nagu.
Aidha, taarifa ya Prof. Nagu imesema hakuna mgonjwa aliyelazwa wala kifo kutokana na ugonjwa huo ulioibuka 2019.
Taarifa ya Prof. Nagu imesema hadi kufikia tarehe 2 Desemba 2022, watu 29,123,387 kati ya walengwa 30,740,928 ambao ni sawa na asilimia 94.7 wamepata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19, ili kuwawezesha wananchi kupata kinga.
“Wizara inawahimiza watu wote wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile homa, mafua, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya viungo, kuumwa kichwa kwenda vituo vya kutolea huduma za afya mapema ili kuweza kupimwa ni kupatiwa matibabu stahiki,”imesema taarifa ya Prof. Nagu.
Leave a comment