April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maambukizi Corona yamshtua mbunge wa Ubungo

Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo (Chadema), ameishauri serikali kutengeneza mikakati ya dharura ya kukabili mlipuko wa Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu, inayosabishwa na Virusi vya Corona (COVID-19). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kubenea ametoa wito huo leo tarehe 2 Aprili 2020, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Mbunge huyo wa Ubungo, ameishauri serikali kutenga fedha za kutosha, kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kujenga maeneo ya kutolea huduma.”Kuna hatari za kiafya za moja kwa moja kutoka nchi tajiri duniani, sembuse sisi Tanzania ambayo hawa jamaa wametupita kwa mbali sana.

Sisi ikilipuka gonjwa hili itakuaje? Mungu atunusuru. Kufanya mdhaha mdhaha hapana.

“Tanzania nzima wanasema kuna vyumba 38 vya ICU ambavyo wagonjwa wa Corona wanatibiwa. Sababu wanatibiwa ama ICU au sehemu yenye mitungi ya Oxgen,” amesema Kubenea.

Wakati huo huo, Kubenea ameishauri serikali kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima, pamoja na kushauri wananchi ambao wanaweza kufanya kazi zao nje ya ofisi, kutekeleza majukumu yao wakiwa nyumbani.

“Jana nimeona picha zinazoonesha msongamano mkubwa katika kituo cha mwendokasi. Nikiangalia hizo picha na tahadhari ambazo dunia inazichukua, tuko katika hatari sana.

“Kama hali ndio hii, na kusanyiko lililotokea jana mtu mmoja akiwa na virusi hivyo athari ya maambukizi inakuaje?” amehoji Kubenea.

Wakati huo huo, Kubenea ameshauri serikali, vyama vya siasa na asasi za kiraia kuungana kwa pamoja katika kukabiliana na janga hilo.

“Huu ni wakati wa kushikamana. Bila kujali dini na kabila ni wakati wa kukaa pamoja na kushikana mikono kwa masilahi ya taifa letu, sio wakati wa kuonyeshana ubabe,” amesema Kubenea.

Pia, Kubenea ameshauri uongozi wa Bunge kusitisha vikao vya mhimili huo, endapo maambukizi ya ugonjwa huo yataongezeka kwa kasi.

https://youtu.be/Ne20tJQLZPw

“Bunge letu linaendelea Dodoma na ninampongeza Spika Job Ndugai kwa hatua alizochukua katika kulinda wabunge na wafanyakazi wa bunge kwa maamuzi haya.

“Amefanya bunge kushiriki wachache ili kuwalinda wabunge, lakini haitoshi, mtu anaweza kuwa mbunge amefunganama jamii akaingia bungeni,” amesema Kubenea na kuongeza:

“Ni vizuri nalo bunge likafungwa kama maambukizi yataendelea, tusione shida kusitisha shughuli za bunge kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu. Ni vyema bunge likajitazama, likatafakari sababu bunge ni chombo cha wananchi linaweza tafuta njia ya kuendelea na shughuli za serikali kupitisha bajeti.”

Kubenea ameishauri serikali kuondoa tozo za kodi kwa wafanyabaishara, ili kupunguza uwezekano wa biashara kufungwa, kitendo kitachoweza hatarisha uchumi wa nchi.

“Ni lazima serikali ichukue hatua ya kufuta baadhi ya kodi katika sekta ya utaliii na hoteli. Zikiachwa hivi, hoteli zitafungwa au kupunguza wafanyakazi.

“Ikiwa hivyo, athari zake ni kubwa na watu watakosa kazi, ni muhimu sana serikali ikaangalia uwezekano wa kuondoa kodi zinazokabili sekta ya biashara, ili biashara na wafanyabiashara waweze kukaa sawasawa katika biashara zao, vinginevyo itakua hasara,” amesema Kubenea.

error: Content is protected !!