June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Uchaguzi mara 100 tutaishinda tu CCM

Spread the love

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amesema hata uchaguzi Zanzibar ukifanyika mara 100, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakitaweza kushinda. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Maalim Seif amesema CCM imeshakataliwa siku nyingi na Wazanzibari ndio maana viongozi wake wamejenga mazoea ya kutumia vyombo vya dola kila unapofanyika uchaguzi ili kutangaziwa ushindi.

Maelezo hayo ni majibu ya swali aliloulizwa na baadhi ya waandishi wa habari la hivi ana wasiwasi gani wa chama chake kushiriki uchaguzi wa marudio wakati amekuwa akijigamba anashinda uchaguzi tangu mwaka 1995 lakini akidai kuwa ushindi huo huwa unaporwa na CCM.

Maalim Seif leo amefanya mkutano mkubwa na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumzia maendeleo ya majadiliano anayofanya na mgombea mwenzake wa urais, Dk. Ali Mohamed, wa CCM, pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar, kuhusu utatuzi wa mgogoro wa kisiasa ulioibuka baada ya matokeo ya uchaguzi kufutwa Oktoba 28, 2015.

Mchana wa siku hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitoa tangazo la kufuta uchaguzi wote akisingizia kuwa ulikumbwa na matatizo yaliyoubatilisha. Alitangaza kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika baadae. Bado Tume haijatangaza tarehe ya uchaguzi mwingine.

Amesema CCM haiwezi tena kushinda uchaguzi kwa sababu imeshakataliwa na wananchi na kuwa sio tena chaguo la Wazanzibari, kutokana na kushindwa kuongoza vizuri.

Amesema CUF haina woga wa kushiriki uchaguzi na akawahakikishia wananchi kuwa kitaendelea kushinda hata ukiitishwa mara 10 iwapo tu utakuwa uchaguzi huru, wa haki na umefanywa katika njia za uwazi.

Maalim Seif ameeleza kuwa hakuna sababu za msingi za kurudiwa kwa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana kwa kuwa hata Tume yenyewe ya uchaguzi ilithibitisha kuwa uchaguzi ulikwenda vizuri mpaka hatua ya kutangazwa kwa matokeo.

Amesema siku ambayo Mwenyekiti wa Tume hiyo alitoa tangazo la kufuta uchaguzi wote Oktoba 28, mwenyewe alikuwa ameshatangaza kura za urais za majimbo 33 na kura za majimbo tisa mengine zilishahakikiwa na kusubiri kutangazwa matokeo yake.

Amesema siku hiyo ilikuwa ndio siku ya tatu tangu tarehe uchaguzi ulipofanyika, na ilikuwa ndiyo siku ya mwisho kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Zanzibar kwa Tume hiyo kukamilisha kutangaza matokeo ya kura za urais.

Amesema Jecha alisubiriwa kikaoni na Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa akiwa na makamishna wa Tume ili kukamilisha kazi ya kutangaza matokeo lakini hakutokea kazini.

“Walipoona makamu mwenyekiti wa Tume alikuwa anaongoza kikao cha kukamilisha kazi ya kuhakiki kura za majimbo yaliyobakia, na kuhisi angetangaza mshindi, walimshinikiza atoe tangazo la kufuta uchaguzi… ni baada ya CCM kubaini wameshindwa uchaguzi kihalali,” amesema Maalim Seif ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho.

Mmoja wa viongozi aliofuatana nao ni Abubakar Khamis Bakary, ambaye ni mwanasheria wa muda mrefu akijulikana kuwa aliongoza kikosi kilichoandika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Maalim Seif alitangulia kusoma taarifa ya maandishi iliyoandaliwa kwa kujumuishwa maelezo ya kisheria ya ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyougubika mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ikiwemo suala la uhalali au uharamu wa uongozi wa Dk. Shein katika kuongoza serikali baada ya muda wake kumalizika Novemba 2, 2015.

Amesema kwa sasa ufafanuzi wa kisheria na katiba unaonesha wazi kuwa kitendo cha Jecha kuvunja Katiba kwa kutangaza kufuta uchaguzi wote pasina kuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo, kimeiweka Zanzibar kuwa nchi isiyo rais halali na serikali halali huku ikiwa pia hakuna chombo cha kutunga sharia, ambacho kwa Zanzibar ni Baraza la Wawakilishi.

Baraza lilimaliza muda wake rasmi kisheria lilipovunjwa Agosti 13, mwaka jana, kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi mkuu, na kulingana na masharti ya Katiba, palitakiwa pawe pamepatikana baraza jipya kufikia Novemba 12, hiyo mwaka jana.

Kufutwa kwa uchaguzi kulikofanywa na Jecha akiwa hakupata ridhaa ya Tume, kwa maana ya idadi inayotakiwa ya makamishna, kumesababisha hata baraza kutokuwepo ingawa washindi wa viti vya uwakilishi kwa majimbo yote 54 walishapewa vyeti vya ushindi.

error: Content is protected !!