July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Tumewashtukia

Spread the love

MGOMBEA wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imepanga kughushi malalamiko ili kujipa uhalali wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika mwandishi Maalum Zanzibar … (endelea).

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo taarifa kuwa, mawakala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na maofisa wa ZEC wamekutana katika Kiwanda cha Makonyo, Wilaya ya Chake Chake kwa ajili ya kujazishwa fomu za malalamiko ili ziweze kutumika kudai kuwa yalikuwepo malalamiko katika zoezi hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za chama hicho zilizoko Mtendeni Mjini Zanzibar, Maalim Seif amesema njama hizo za CCM wameshazigundua na hawatozikubali.

Amesema, njia pekee ya kuondoa utatanishi wa uchaguzi huo ni kukamilisha uhakiki wa majumuisho na kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Amesema kwa upande wake pamoja na chama chake, wataendeleza jitihada za kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kukamilisha uhakiki wa majumuisho ya kura kwa majimbo 14 yaliyobaki na hatimaye kutangazwa mshindi wa urais hadi ifikapo tarehe 02 Novemba mwaka huu.

Hata hivyo amesema iwapo hakutokuwa na hatua zozote zilizochukuliwa kukamilisha uchaguzi huo na kuheshimu maamuzi ya wananchi walio wengi hadi ifikapo siku hiyo, viongozi wa CUF wataondoa mkono wao na kuwaachia wananchi waweze kutafuta haki yao kwa njia za amani.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kuwatesa na kuwapiga raia wasiokuwa na hatia katika makaazi yao.

Amesema matukio hayo yamekuwa yakiripotiwa zaidi katika Wilaya za Magharibi “A na B”, na katika tukio la hivi karibuni amesema nyumba za raia wasiokuwa na hatia zimechomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu na kuwafanya wananchi kuanza kupoteza uvumilivu.

Wakati huo huo Sarafina Lidwino anaripoti kuwa, CUF jijini Dar es Salaam imeeleza wasiwasi wake wa kutokea machafuko iwapo ZEC itaendelea ‘kubana’ matokeo.

Chama hicho kimeeleza kugomea uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha wa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo uliofanyika 25 Oktoba mwaka huu.

Uchaguzi huo umekuwa na upinzani mkubwa kati ya Chama cha Wananchi (CUF) kilichomsimamisha Maalim Seif Shariff Hamad na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichomsimamia Dk. Ali Mohamed Shein.

Siku moja baada ya upigaji kura, Maalim Seif aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba, amepata kura nyingi kwenye uchaguzi huo ambapo takwimbu hizo aliziweka hadharani.

CUF imeeleza kuwa kitendo cha kutotangaza matokeo ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za Zanzibar ambapo wamemtaka Jecha kubatilisha uamuzi wake hivyo kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam katika ofisi za chama hicho, Mwenyekiti Kamati ya Uongozi, Twaha Taslima amesema chama chao kimepitia katiba za uchaguzi zote ya Tanzania Bara na Zanzibar na kujiridhisha kuwa, Jecha amevunja katiba.

“Tumepitia Katiba ya Tanzania ya 1977, Katiba ya Zanzibar 1984, sheria ya Uchaguzi sura 343 ya mwaka 2010, sheria ya Zanzibar Na. 11 ya 1984 na kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za 2015 na kujiridhisha kuwa, hakuna kifungu chochote kinachozipa mamlaka NEC na ZEC kufuta uchaguzi uliofanyika.

“Kinachosikitisha zaidi Jecha alichukua uamuzi binafsi bila kuwashirikisha watendaji wenzake kutoka Zanzibar na hata NEC pia hakuishirikisha, hiyo ina maana kwamba alifanya maamuzi kwa shinikizo la Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuona kimeshindwa kuchaguliwa na wananchi,” amesema Taslima.

Aidha, katika taarifa ya Jacha iliyotolewa juzi ilieleza kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu ulikabiliwa na vikwazo vingi ambavyo alidai ndivyo vilivyomchochea kufuta uchaguzi huo na kudai kutokana na mamlaka aliyonayo, anauwezo wa kufuta.

Taslima amesema, tangazo hilo lilizua sintofahamu hasa pale ambapo ilibainika kuwa, hata Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kusema hatambui uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar.

“CUF kimesikitishwa na kinalaani hatua hiyo iliyofanywa na Jecha kwani inaweza kuanzisha mtafaruku mkubwa na kusababisha uvunjifu wa amani nchini. Tunawataka wasimamizi wa nje kulisimamia jambo hilo na kuhakikisha wananchi wanapata haki yao,” amesema.

Kuhusu matokeo ya urais yaliyotangazwa jana na Jaji Lubuva kwamba mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ameshinda urais amesema, CUF wanaungana na msimamo uliotolewa jana na mgombea urais anayewakilisha UKAWA, Edward Lowassa wa kutotambua matokeo hayo.

Taslima amesema ikumbukwe kuwa, CUF pia ni miongoni mwa Ukawa na kwa msingi huo, “basi tunaungana na uamuzi wa mgombea wetu Edward Lowassa wa kutokubaliana na matokeo yaliyotangazwa na NEC kuwa ni batili.”

error: Content is protected !!