July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Sinunuliki

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad amesema yeye si mwanasiasa mwepesi wa kuweza kununuliwa na hakuna kiongozi hata mmoja kutoka CCM aliyepata kumfikia kwa lengo hilo, anaandika Jabir Idrissa.

“Kama yupo kiongozi yeyote mwenye uhakika kuwa mimi ninanunlika ajitokeze hadharani,” alisema wakati akijibu swali la kushukiwa kuwa anatumika kuendeleza hujuma ya maamuzi ya wananchi wa Zanzibar.

Maalim Seif leo amefanya mkutano na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Hyatt ya mjini Zanzibar kueleza msimamo wake wa kutomtambua Dk. Ali Mohamed Shein kuwa rais wa Zanzibar na kuahidi kushikilia msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF.

Tarehe 4 Aprili uongozi wa CUF ulitoa tamko hilo kuzidi kuthibitisha msimamo wa chama hicho kutotambua maamuzi yote yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuanzia ile hatua ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha kutangaza 28 Oktoba 2015 kufuta uchaguzi mkuu uliofanyika 25 Oktoba.

Baada ya Jecha kutoa tangazo hilo, siku ambayo Tume ilitarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya uchaguzi ambao asasi za uangalizi ziliusifia kuwa ulikuwa huru na wa haki na uliokidhi matakwa ya wananchi, Jecha alitangaza alichoita “uchaguzi wa marudio” ambao CUF iliugomea.

CUF iliita uchaguzi wa Jecha kuwa ni haramu na ikasema haiashiriki na tayari imewapongeza wananchi kwa kuitikia wito wa kuoshiriki, kwani vituo vya uchaguzi vilionekana kukosa wapigakura.

Jecha alitangaza matokeo ya uchaguzi huo siku ya pili tu akisema Dk. Shein ameshinda kwa kupata kura 299,982 ikiwa ni asilimia 91.2 ya kura 341,865 zilizopigwa.

Tangu Jecha ambaye ni kada wa CCM aliyegombea nafasi ya kuteuliwa kuwania ubunge kupitia chama hicho uchaguzi wa 2010, alipoufuta uchaguzi wa Oktoba 2015, Maalim Seif na CUF wamekuwa na msimamo kuwa waliporwa ushindi ikiwa ni hatua mbaya ya Jecha kutumiwa na CCM kuhujumu maamuzi ya wananchi.

Lakini kumekuwa na baadhi ya makada wa CCM wanaoeneza taarifa kuwa Maalim Seif hajasema ukweli kuwa amekubali kusalimu amri kudai haki yake kwa kuwa amenunuliwa na viongozi wa CCM.

Na hilo likawa swali la Mhariri wa gazeti la MwanaHALISI, Jabir Idrissa aliyehudhuria mkutano wa waandishi wa habari mjini Zanzibar akitaka kiongozi huyo aseme kama amekuwa na bei katika harakati za kutaka kuiongoza Zanzibar.

“Sinunuliki… sina bei na kwa kweli hakuna bei ya kuninunua mimi. Siku zote nimekuwa imara katika misingi ninayoiamini ya kufanya siasa makini kwa kuwa naamini katika ukweli, uadilifu na haki katika kutafuta uongozi,” alisema.

Alisema hayuko tayari kuhalifu dhamira yake ya kuongoza Zanzibar na kwamba ataendelea kupambana chini ya misingi ya demokrasia, sheria na kujali haki za watu ambao tayari wameshamthibitishia kuwa wamempa ridhaa yao awaongoze.

Maalim Seif amesema CUF itaendelea kudai haki ya wananchi kwa njia za kidemokrasia, Sheria na Katiba huku wakihimiza wananchi kudumisha amani na utulivu katika nchi.

Kuhusu hatua ya Dk. Shein kupuuza msimamo huo akiwa tayari ameshaunda serikali kwa kutangaza baraza la mawaziri jana, na kwamba hana hofu ya kutotambuliwa na CUF kwa kuwa anatambuliwa na Mwenyezi Mungu, Maalim Seif amesema kwanza Dk. Shein athibitishie ulimwengu kuwa amekutana na Mungu akamweleza kuwa anamtambua.

Kwa upande mwingine amesema maneno ya kiburi na jeuri hayo yanatoka sasa wakati ukweli ni kwamba amesema Dk. Shein anajua hana uwezo wa kuiendesha serikali inayosusiwa misaada kama alishindwa ikiwa na misaada iliposhindwa kukidhi hata bajeti ya mishahara na shughuli nyingine za utawala kutoka 2010 hadi 2015.

SOMA HOTUBA KAMILI HAPA

error: Content is protected !!