January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Ramadhani hii bei juu

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa sokoni kuangalia bidhaa

Spread the love

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema, upungufu wa bidhaa katika masoko mbalimbali visiwani Zanzibar umechangia kupanda kwa bei za bidhaa hizo. Anaandika mwandishi wetu … (endelea).

Amesema, tofauti na Ramadhani iliyopita, Ramadhani hii kumekuwepo upungufu wa bidhaa zinazotumika zaidi kwa futari ikiwemo ndizi, viazi vikuu na majimbi hali iliyochangia bei ya bidhaa hizo kuwa juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi.

Maalim Seif ameeleza hayo leo katika ziara yake ya kutembelea masoko mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kuangalia hali ya upatikanaji wa bidhaa za matunda na nafaka ambazo hutumika zaidi katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa ajili ya futari. 

Masoko aliyoyatembelea ni pamoja na Soko la Matunda Mombasa, Mwanakwerekwe, eneo la biashara Saateni, Soko la Samaki Malindi na Darajani.

Amesema, upungufu huo wa bidhaa unaweza kuchangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo kiangazi cha muda mrefu, pamoja na mafuriko yaliyotokea Tanzania Bara ambapo bidhaa kutoka mikoani zinachelewa kufika katika masoko ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Hata hivyo ameelezea matumaini yake kuwa, bei ya bidhaa hizo zinaweza kushuka na kuwanufaisha wananchi iwapo zitapatikana kwa wingi katika masoko. 

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa samaki amesema, bei ziko juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi, na kutoa wito kwa wafanyabiashara wa samaki kuzingatia hali hiyo.

Katika eneo la biashara Saateni, Maalim Seif amesema bado eneo hilo linakabiliwa na upungufu wa wateja licha ya baadhi ya wafanyabiashara kuitikia wito wa kuendelea kufanya biashara katika eneo hilo.

Baadhi ya wafabiashara wa eneo hilo la Saateni wamesema miundombinu ya eneo hilo hairidhishi, na hivyo wateja wengi kushindwa kufika kununua bidhaa zao.

Wamezitaja kasoro kubwa zinazochangia hali hiyo kuwa ni kutokuwepo kituo cha daladala katika eneo hilo, na kwamba wateja wao hupata usumbufu wanapotaka kwenda eneo hilo.

Hivyo wameliomba Baraza la Manispaa kuimarisha miundombinu hiyo ili kuliweka eneo hilo katika mazingira mazuri ya kibiashara. 

Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar, Abeid Juma Ali amekiri kuwepo kwa kasoro hizo lakini amesema tatizo la kufika kwa gari za abiria linatokana na madereva, kwani baraza hilo tayari limeshaweka utaratibu wa kuwepo kwa kituo hicho.

error: Content is protected !!