September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Prof. Lipumba ‘stop’

Spread the love

JUHUDI za Prof. Ibrahim Lipumba, kurejea katika nafasi yake ya uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), zimegonga mwamba, anaandika Pendo Omari.

Maalim Seif Sharif Hamad, katibu mkuu wa chama hicho taifa, “amekataa kubariki” hatua za Lipumba kurejea katika nafasi hiyo; hata kuwania nafasi nyingine yoyote katika chama.

Maalim amekaririwa akisema hayo wakati wa kujibu swali la mmoja wa waandishi wa habari wa Tanzania anayefanya kazi zake nchini Marekani.

Alisema, Prof. Lipumba “alijuzuulu mwenyewe miezi minane iliyopita. Hakulazimishwa; yeye mwenyewe alionyesha nia ya kutaka kujiuzulu.”

Anasema, “watu wengi, wakiwamo wazee na mashekhe, walimfuata kumuambia tafadhali usijiuzulu; lakini akaendelea na azma yake. Akajiuzulu.”

Maalim Seif anasema, Prof. Lipumba hakushindikizwa na mtu kujiuzulu, barua yake aliipokea na kuipeleka kwenye Baraza Kuu la Uongozi (BKU) ambako wajumbe kwa kauli moja, wakaridhia kuachia ngazi.

“Baraza Kuu wakaipokea taarifa ile, wakachagua Kamati ya Uongozi ya muda ya kuongoza chama mpaka hapo atakapo patikana mwenyekiti mpya. Kamati ile bado ipo na Maalim Seif hana uwezo wa kuiondoa.”

Akiongea kwa sauti ya ukali, Maalim Seif alisema, “Kamati ile imewekwa na Baraza Kuu la uongozi la taifa. Haiwezi kuondolewa na Maalim Seif na huwezi kuwa na uongozi juu ya uongozi.”

Msimamo wa Maalim Seif unashahabiana na ule wa Naibu Katibu mkuu wa CUF Visiwani, Nassor Ahmed Mazrui, anayesema kuwa Prof. Hana nafasi katika chama chake.”

Anasema, “Prof. Lipumba hana nia njema. Anataka kuja kuiharibu CUF. Anataka kuharibu mipango yetu.”

Akiwa anahaha kurejea katika nafasi yake ya uenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba amesema ameamua kurejea tena katika nafasi yake kutokana na “kuombwa na makundi ya wanachama na viongozi wa dini…”

Amesema ametafakari kwa kina maombi hayo huku akizingatia hali halisi ya siasa ya Visiwani ambayo kwa sasa si shwari.

Uamuzi huo anasema, ameuchukua kwa kuzingatia Ibara ya 117 ya katiba ya CUF inayoelezea kwa undani jinsi kiongozi anavyoweza kujiuzulu na kurejea tena ndani ya chama hicho.

Taarifa zinasema juhudi za Prof. Lipumba kurudi kileleni zinalenga kuvunja nguvu za Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) zilizodhihirika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya CUF zinasema, shinikizo la kutaka Prof. Lipumba kurejea katika nafasi yake bila kufanyika uchaguzi, linatokana na baadhi ya wapambe wake kunusa kuwa kiongozi huyo hawezi kushinda katika uchaguzi wa ndani ya chama.

“Baada ya kuona Prof. Lipumba hawezi kushinda uchaguzi, viongozi wake wawili (majina tunayo), wakatengeneza mkakati ili arejeshwe katika nafasi yake,” ameeleza kiongozi mmoja wa chama hicho aliyeko Buguruni, Dar es Salaam.

Amesema, “lakini nataka nikuambie, Prof. Lipumba hana tena nafasi ndani ya CUF. Kuruhusu Prof. Lipumba kurejea CUF akiwa mwenyekiti ni kutaka kuangamiza Ukawa. Nasi tunajua kuwa Ukawa umeumiza sana CCM. Hatutakubali.”

Prof. Lipumba alijivua nafasi ya mwenyekiti Agosti mwaka jana, katikati ya vuguvugu la uchaguzi mkuu, huku mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa akitikisa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichosimamisha John Pombe Magufuli.

Kwa habari zaidi juu ya sakata la Prof. Ibrahim Lipumba na chama chake, soma gazeti la MSETO la kesho Alhamisi-(MHARIRI).

error: Content is protected !!