MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema, atapiga kura siku ya kwanza kesho Jumanne tarehe 27 Oktoba badala ya siku ya uchaguzi Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Maalim Seif amesema hayo leo Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2020 wakati anazungumza na waandishi wa habari kuhusu kura ya mapema inayofanyika kesho kwa watumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na watumishi watakaosimamia siku ya uchaguzi mkuu.
Mwanasiasa huyo amesema, atapiga kura katika Kituo cha Garagara na atawasili kituoni hapo saa 2:30 asubuhi.
“Mimi napiga kura katika Kituo cha Garagara na nategemea kesho saa 2:30 asubuhi kwenda kupiga kura. Ni haki yangu,” amesema Maalim Seif.
Maalim Seif amesema, uamuzi wakupiga kura ya mapema unatokana na ZEC kushindwa kutoa takwimu za wapiga kura ya mapema.
“Kwa kuwa ZEC imeshindwa kutoa takwimu za Wapiga kura ya mapema na pia, kushindwa kuweka wazi majina ya wapigakura hadi sasa, niwatake wananchi wote kujitokeza kwa wingi kesho Jumanne katika vituo vyote vya kupigia kura. Wananchi wote wajitokeze kwa amani, bila vurugu na kudai haki ya kupiga kura kwa amani,” amesema Maalim Seif.
Aidha, Maalim Seif amewataka wananchi watakaoshindwa kupiga kura kesho wajitokeze kutimiza wajibu wao huo Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020.
“Pamoja na kuwepo kwa masuala mengi yasiyo na majibu mpaka sasa kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, hali inayothibitisha mashaka yetu kuwa ZEC haipo kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa wazi.”
“Wazanzibari wanapaswa kufahamu ni umoja wetu na mshikamano wetu ndio utakaoleta mabadiliko ya kweli nchini,” amesema Maalim Seif.
Leave a comment