July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Namhurumia Dk. Shein

Spread the love

TAREHE 20 Machi 2016, kulifanyika uchaguzi wa marudio wenye utata katika visiwa vya Zanzibar, ambao ulisuswa na chama kikuu cha upinzani visiwani humo, Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar (CUF).

Aliyetangazwa mshindi ni Dk. Ali Mohamed Shein, rais aliyegombea akiwa madarakani, akashindwa kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015 ambao Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), badala ya kutangaza mshindi, akaufuta kinyume cha sheria, na kusababisha mgogoro mpya wa kisiasa.

Tayari Dk. Shein ameapishwa kuongoza Zanzibar kwa ngwe nyingine ya miaka mitano. MwanaHALISI lilifanya mazungumzo na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, ambaye aligomea uchaguzi wa marudio.

Yafuatayo ni maswali na majibu kati yake na gazeti hili, Jumatano iliyopita, siku moja kabla ya Dk. Shein kuapishwa, kama yalivyoandikwa na mwandishi wetu, Josephat Isango.

MwanaHALISI: Uchaguzi umefanyika Zanzibar na nyie mlitoa msimamo kuwa hamtashiriki na kweli hamkushiriki. Nini kinafuata sasa?

Maalim Seif: Nitajibu kwa namna mbili: Kwanza, CCM wamwapishe rais wao, watamwapisha Dk Shein na yeye ataunda serikali yake ataendelea.

Pili, tunasema Uchaguzi wa 20 Machi haukuwa halali, uchaguzi huru na wa haki ulifanyika Oktoba 25, wala Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salimu Jecha hakuwa na mamlaka kisheria ua kikatiba ya kufuta, yote yaliyofuata ni haramu sisi tulitangaza hatutashiriki lakini pia hatutaitambua serikali iliyoundwa baada ya uchaguzi wa marejeo na hatutaipatia ushirikiano wa namna yeyote ile.

MwanaHALISI: Huko nyuma mlikuwa mnafanya siasa ndani na nje, safari hii hamtakuwepo kwenye baraza la wawakilishi, mtaendeshaje harakati za kudai haki ndani ya Zanzibar?

Maalim Seif: Hili siyo la mwanzo, lilishawahi kutokea. Wenzetu waliwahi kulazimisha uchaguzi katika majimbo kadhaa ya Pemba, na sisi tulishiriki kwa aina yake, wananchi walipiga kura za maruhani.

Utakuta mwakilishi anachaguliwa kwa kura mia mbili, au mia moja tukawa hatupo katika baraza la wawakilishi, wakati wa Rais Dk. Salmini Amour, vile vile tulisusia, wawakilishi wetu hawakuwepo lakini chama cha CUF kiliimarika.

Sasa mara hii tunasema hatumo katika Baraza lakini tumo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, na wabunge wetu wapo tena wengine ni mawaziri vivuli, kwa hivyo siasa tutaifanya vizuri maana kila chama kinapopata mitikisiko ndipo kinaimarika zaidi na wananchi wanakuwa na ari zaidi kukijenga chama chao.

MwanaHALISI: Kule Zanzibar hivi sasa wananchi wanasubiri kujua nini kinafuata baada ya uchaguzi, na CCM wamechukua hata majimbo mliyokuwa nayo ya wawakilishi na madiwani, unawaambiaje sasa wananchi wa Zanzibar?

Maalim Seif: Nawaambia wananchi wa Zanzibar CUF tunaaamini katika amani, tusifanye jambo lolote litakaloharibu au kuchafua amani ya nchi, sisi bado tunazo njia za kuendeleza mapambano haya kwa amani.

Hatuitambui serikali, hatushikirikiani nayo, na hatuko tayari kufanya lolote na serikali ya Dk. Shein, tutaipinga ndani na nje.

MwanaHALISI: Migogoro Zanzibar imekuwa ya muda mrefu na ya kihistoria. Umetafuta urais kwa miongo miwili, sasa nini kinaweza kunusuru Zanzibar kisiasa?

Maalim Seif: Nilidhani maridhianao ya Wazanzibar ya mwaka 2009 ambayo yalifikiwa baada ya mimi na Dk. Abeid Aman Karume, (Rais wa Awamu ya Sita) kukubaliana kwamba yaliyopita yamepita tuanze ukurasa mpya.

Nilishuhudia akimaliza muda wake alisema atahakikisha uchaguzi uliofanyika unakuwa huru na haki, kwa kiasi kikubwa huu haukuwa wa haki, ulikuwa wa vitisho vya majeshi na matumizi ya nguvu.

Wakati ule kila mtu alipiga kura na tukaunda serikali ya kitaifa, na nyie ni mashahidi kwa miaka mitano tulikwenda vizuri. Hasama zote zilizokuwepo na migogoro ilimalizika Wazanzibar wakashirikiana bila kujali tofauti za itikadi za kisiasa.

Walifanya kazi kwa mashirikiano makubwa. Ni jambo la kusikitisha kwani kwa kile ambacho CCM wanasema lazima washinde, wamekataa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, hawana sababu yeyote, sababu zote ni za kupika na muda wote tukiwaambia leteni ushahidi, walishindwa.

Lakini sababu wanasema hawawezi kukubali wapinzani kuongoza Zanzibar, walimtaka na kumlazimisha Jecha afute uchaguzi ule na kuandaa uchaguzi mpya, hivyo mgogoro huu chanzo ni CCM.

Pia mimi nilidhani tulishapita huko lakini kwa kuwa CCM wanataka ni lazima washinde, isiposhinda inaonekana haukuwa wa kidemokrasia, kwa kweli inasikitisha. Wameturejesha miaka 20 nyuma na sasa katika baadhi ya maeneo tayari hasama zimeshaanza.

Watu wa itikadi tofauti hawashirikiani kwa lolote hata kama kwenye masuala ya mazishi.

Tofauti ni kwamba hawa wenzetu (CCM) wanaangalia suala la madaraka tu lakini masuala mapana ya maslahi ya nchi hawana habari nayo, sisi hatukubali hivyo.

Otherwise (vinginenvyo) wafute mfumo wa vyama vingi, wabaki na chama kimoja, lakini kama kuna mfumo wa vyama vingi basi kuna kushindwa na kushinda. Haiwezekani wao lazima washinde.

Hatuwezi kukubali hili maana tukikubali na kuacha mambo yaende yanavyoenda, inawezekana mwaka 2020 upinzani unaweza kushinda huku bara lakini CCM wakakataa.

Tumeona mfano mzuri katika sakata la uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar hadi Rais John Magufuli alipotoa kauli ndio CCM wakarudi nyuma.

Hatukubali kabisa, hili halitaishia hapa, tutatetea haki za wananchi, tutatetea maamuzi yao kwa njia za amani kabisa.

MwanaHALISI: Inaonekana kuwa katika matokeo yaliyotangazwa na tume, Wazanzibari walijitokeza kwa wingi kupiga kura hata wale wa Pemba ambapo ni ngome ya CUF.

Maalim Seif: Kila kitu kilishapikwa hata kabla ya uchaguzi, tunashukuru baadhi ya vyombo vya habari vilionyesha jinsi hali ilivyokuwa, sio Pemba tu bali hata Unguja.

Unguja walijitokeza wanawake tena wazee, lakini wanaume na vijana hawakuonekana, ila tukasema hawa watapika matokeo. Ushindi tuliopata ni kuwa watu waliitikia wito wetu, na kweli hawakujitokeza kupiga kura.

Namhurumia kweli Dk. Shein, ikiwa anaamini kapata kura zile anajidanganya, maana hata alipopiga kura yeye alizungukwa na vikosi tu lakini wananchi walikuwa wachache.

Wazanzibar waliitikia wito wetu, hawakwenda kupiga kura, na wengi wao waliungana. Tuliambiwa wengine walipewa kura sita hadi kumi ili watumbukize tu, masuala yalikuwa wazi. Jecha alitangaza matokeo feki, ni yao ya kujidanganya.

MwanaHALISI: Je, mmeshawasha taa kabisa kuwa hamtashiriki tena uchaguzi kama siasa za Zanzibar zinaenda kama CCM wanavyotaka, unadhani nini kifanyike?

Maalim Seif: Kama yatatokea maridhiano yatakayoongozwa na kusimamiwa na vyombo na taasisi huru za kidemokrasia, bila vitisho vya majeshi na polisi – vyombo vya dola vikae pembeni – kuwa na vyombo huru vya habari vinavyotenda haki na tume huru, sio hii iliyopo Zanzibar chini ya Jecha, hapo CUF kitaweza kufikiri kushiriki uchaguzi.

MwanaHALISI: Msimamo mkali wa CUF juu ya muundo wa muungano unawezekana ndio unaipa hofu CCM ambayo umesema imekuwa haikubali kuacha madaraka visiwani Zanzibar, labda huo msimamo wenu mkali kabisa juu ya muundo wa muungano wa kuitaka Zanzibar yenye mamlaka kamili ndio hofu kuu ya CCM na Mpo tayari kubadilisha msimao wenu?

Maalim Seif: Mimi niseme visingizio tu hivyo; hata nilipokutana na Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuondoka, aliniambia, “Maalim, CCM inakuogopa.” Nikamuuliza, “kwanini waniogope?” Akasema, “kwa sababu utavunja muungano!” Mimi nikamuuliza, “Rais, hivi na wewe unaamini kweli mimi naweza kuvunja Muungano?

Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye mwenye vyombo vyote, ndiye mwenye jeshi, polisi, usalama wa taifa na vyombo vyengine. Rais wa Zanzibar ana nini? Sasa vipi huyu mtu dhaifu hana chochote atavunja Muungano?”

Kwa hivyo, hizi ni sababu tu. Lakini niseme tu, kwamba Muungano hautovunjwa na CUF. Muungano utavunjwa na CCM. Haiwezekani kabisa kabisa kabisa Wazanzibari kila mwaka wanafanya maamuzi halafu Serikali ya Muungano na CCM Bara wanaingilia, wanawapa watu ambao wamekataliwa. Hivi unadhani leo waulize Wazanzibari, wangapi wana imani na Muungano? Ikiwa wanataka Muungano wa majeshi, well and good (sawa, vizuri), lakini mimi naamini katika Muungano ambao umo kwenye nyoyo za wananchi.

Hasa kwa vitendo ambavyo wanatufanyia wenzetu CCM wa Bara, Wazanzibari hawawezi kuwa na imani na Muungano huo hata siku moja; kwamba hawa hatuwataki, ninyi mnalazimisha hao hao, halafu unatazamia Mzanzibari awe na imani na Muungano! Kwa hivyo, Muungano utavunjwa na CCM, tena CCM Bara na Serikali ya Muungano.

MwanaHALISI: Kwanini unaamini CCM Bara wanataka kuvunja Muungano?

Maalim Seif: Wao wanavyosema hawataki. Wanataka kulazimisha, lakini watavunja Muungano, kwa sababu ya vitendo vyao kama nilivyosema. Muungano lazima uwe katika nyoyo za wananchi. Huu Muungano ambao wanasema wa kulazimisha, wataweka majeshi miaka nyote kule Zanzibar, vitendo hivyo ndivyo vitakavyosababisha Muungano kudhoofika na mwisho kuvunjika.

error: Content is protected !!