Friday , 9 June 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif: Naingia Ikulu 2020
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif: Naingia Ikulu 2020

Spread the love

MAALIM Seif Sharif Hamad, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, amejigamba kuingia Ikulu ya Zanzibar baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 27 na 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Ametoa kauli hiyo jana Jumapili tarehe 13 Septemba 2020, katika uzinduzi wa kampeni za urais za chama hicho, uliofanyika kwenye uwanja wa Demokrasia – Kibanda Maiti, Unguja.

“Niseme tumeanza rasmi safari yetu ya kuelekea Ikulu, juzi baada ya ZEC (Tume ya Uchaguzi Zanzibar), kuniteua kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar na sasa gari tushaitia moto injini, inawaka hatusimami mpaka Ikulu. Ni lazima ushindi wetu utufikishe Ikulu,” alisema Maalim Seif.

Akielezea ahadi zake, Maalim Seif alisema, akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atahakikisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaimarika.

“Kila mgombea anajipendekeza ataenzi muungano, muungano upi? Sisi tuko wazi, tunataka muungano wa haki na usawa,” ameahidi Maalim Seif.

Aidha, Maalim Seif alisema, kipaumbele chake cha kwanza kitakuwa ni uimarishaji wa utawala wa sheria pamoja na mihimili ya nchi ili kila mmoja ufanye kazi yake kwa ufanisi bila kuingiliana majukumu.

“Nitaje tu jambo la kwanza ambalo tunahisi muhimu katika nchi ni suala zima la utawala au uongozi katika nchi, tunahitaji nchi inayoongozwa na Katiba na Sheria, Utawala wa Sheria utawale katika nchi yetu,” alisema Maalim Seif.

“Lazima tutambue kuna mihimili mitatu ya nchi, Baraza la Wawakilishi, Mahakama na Serikali yenyewe, hii ni mihimili mitatu lazima kila mhimili uheshimu mihimili mingine, kila mhimili ufanye kazi kwa kujitegemea yenyewe.”

Mgombea huyo, alisema katika serikali yake majaji na mahakimu hawatatekeleza majukumu yao kwa matakwa ya wanasiasa, bali kazi yao itakuwa ni kutoa haki bila shinikizo kutoka kwamtu yeyote.

Na kwamba, kama atashinda uchaguzi huo, katika serikali yake hatakuwa na mamlaka ya kuteua majaji ili kuondoa mgongano wa masilahi, bali litaundwa jopo maalum la wataalamu wabobezi wanaoaminika na wenye heshima kwa jamii, ambalo litakuwa na kazi ya kuteua viongozi hao wa mahakama.

“Majaji chini ya uongozi wa ACT Wazalendo hawatachaguliwa na rais, rais atawatamka tu lakini kutakuwa na jopo la watalaamu wabobezi wanaoaminika, wenye heshima katika jamii, hao watateua na kumshauri rais, majaji hawa watakuwa huru hawataogopa sababu rais amewateua, “ alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema, kwenye Serikali yake Baraza la Wawakilishi litakuwa na mamlaka ya kusimamia na kuishauri Serikali. Pia, Serikali yake itaendeshwa kwa uwazi.

“Tunataka wabunge wasio mabubu watakaotetea wananchi wao, Serikali yangu kwanza itakuwa inayoendesha mambo yake kwa uwazi, kila mtu atakua na haki kujua nini Serikali inafanya, Serikali itakayoongozwa na Maalim vyombo vya habari vitakuwa na uhuru wa kukosoa hawatafungwa midomo,” alisema Maalim Seif.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Ngoma bado mbichi mkataba wa Bandari

Spread the love  SAKATA la mkataba wa uendeshaji, uendelezaji na uboreshaji wa...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mkataba unaweza kuvunjwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

BiasharaTangulizi

Mkurugenzi TPA: Mikataba ya utekelezaji bado haijasainiwa

Spread the loveMKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),...

Habari za Siasa

Lussu: Mkataba wa DP bandarini si wa miaka 100

Spread the loveMAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amesema hakuna ukweli wowote...

error: Content is protected !!