MAALIM Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa Chama cha siasa cha upinzani cha ACT-Wazalendo nchini Tanzania amesema, msajili wa vyama vya siasa nchini humo hawezi kufuta usajili wa chama hicho kwa sababu ni kinyume ch sheria. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam…(endelea).
Maalim Seif ameyasema hayo leo Ijumaa tarehe 17 Julai 2020 alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho jimbo la Mbagala jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Maalim Seif ambaye amechukua na kurejesha fomu ndani ya chama hicho kuomba kupitishwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar amesema, licha ya kuwepo kwa tishio la kufutwa kwa chama hicho lakini msajili hataweza kufanya hivyo kutokana na sheria ya vyama vya siasa inamzuia kukifuta chama mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.
Soma zaidi hapa
Msajili aikamia ACT-Wazalendo, atishia kuifuta
Mkongwe huyo wa siasa nchini amesema hisia zake kuwa barua hiyo imekuja kwa lengo la kuwatisha wananchi wasijiunge na chama na chama hicho.
“Madai yake ya tangu mwaka 2018 na yote tushajibu na hakuna sehemu moja aliyesema hajaridhika,” amesema

“Kwanza niwatoe wasiwasi wanachama, hawawezi kufuta chama sheria ya nchi inasema tena kaitunga yeye kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja kabla ya uchaguzi huwezi kukifuta chama kwa hivyo chama chetu kipo salama,” amesema
Wakati huo huo Maalim Seif amewaonya viongozi wa chama hicho kutojihusisha na vitendo vya rushwa hususan wakati huu kwenye uchaguzi.
Amesema moja ya miiko ya chama hicho ni mgombea kutumia majina vya viongozi kuwa ametumwa na kiongozi fulani achukue fomu.
Soma zaidi hapa
Zitto amjibu Msajili vyama vya siasa
Amesema mgombea atakayekwenda kinyume na sheria za chama ataenguliwa na vilevile kwa kiongozi atakayejihusisha na matendo hayo atatolewa kwenye nafasi yake.
Kauli ya Maalim Seif kuhusu kufutwa chama hicho ameitoa ikiwa ni siku takribani tatu kupita tangu msajili wa vyama vya siasa kukiandikia barua chama hicho kuelezea ukiukwaji wa sharia ya vyama vya siasa na hatua ambazo atazichukua.
Barua hiyo iliyoandikwa tarehe 14 Julai 2020 na kusainiwa Sisty Nyahoza, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa imeeleza kusudio lake la kutaka kukipa adhabu ACT-Wazalendo kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.
“Kutokana na ukweli kwamba, tangu mwaka 2018 ACT-wazalendo mmefanya vitendo kadhaa vya kukiuka sheria ya vyama vya siasa na msajili wa vyama vya siasa amekuwa akiwaasa muache kufanya hivyo, lakini hamzingatii ushauri wake,” imeeleza barua hiyo
“Msajili wa vyama vya siasa anakusudia kuwapa adhabu chini ya sheria ya vyama vya siasa, ili iwe fundisho kwenu na kwa vyama vya siasa vingine kuwa, ni muhimu kuheshimu Sheria za nchi ikiwamo sheria ya vyama vya siasa katika shughuli za kisiasa na vyama vya siasa, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi.”
Leave a comment