January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif kuanza safari Ikulu

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad, mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika siasa Tanzania, ataanza safari ya kutwaa madaraka ya dola Jumapili atakapochukua fomu ya uteuzi ya kugombea urais wa Zanzibar. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Mgombea wadhifa huo mara ya tano mfululizo Maalim Seif anatarajiwa kuchukua fomu hiyo makao makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mjini Zanzibar asubuhi saa 3:00.

Taarifa ya Meneja wa kampeni yake, Nassor Ahmed Mazrui, imesema mara tu akishachukua fomu, Maalim Seif atakuwa na mkutano kwenye ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani ambako wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wamealikwa kuhudhuria.

Mazrui ambaye naye atagombea kiti cha uwakilishi jimbo jipya la Mtopepo, amesema katika mkutano huo Maalim Seif anatarajiwa kutoa alichokiita “Maelezo ya Utangulizi” ya sababu zilizomchochea kuendelea kugombea urais wa Zanzibar mfululizo tangu mwaka 1995.

Katika mwaka huo, Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa au Government of National Unity (GNU), aligombea kwa mara ya kwanza katika mfumo wa siasa za vyama vingi baada ya kurudishwa kupitia Sheria ya Bunge mwaka 1992 mara hii siasa ikifanywa suala la Muungano.

Zanzibar na Tanganyika zilizoungana kupitia Muungano wa Aprili 26, 1964, kila moja ilikuwa na harakati za namna yake kutafuta ukombozi kutoka utawala wa wageni. Kila upande ulikuwa na vyama vyake vya siasa, Zanzibar ikitegemea Afro-Shirazi (ASP) na Tanganyika chama cha TANU.

Maalim Seif ameshiriki kugombea urais katika uchaguzi wa 2000, 2005 na 2010, ambapo mara zote hizo, yeye na Chama cha Wananchi (CUF) anachokiwakilisha akiwa sasa Katibu Mkuu, wamekuwa na msimamo kuwa wanaporwa ushindi kwa mtandao mahsusi unaohusisha wanausalama walioko ndani ya Tume ya Uchaguzi, vyombo vya serikali na wakitumiwa na viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mara zote uchaguzi umekuwa ukifanyika chini ya mazingira ya vitisho na kampeni zilizojaa chuki huku viongozi wa CCM wakitumia kila mbinu kujihakikishia ushindi hata kama ni kwa gharama za maisha ya wananchi.

Baada ya mara nne kushindwa kushika dola kupitia uchaguzi wa kidemokrasia, kwa kuwa unavurugwa kimkakati, Maalim Seif amesema mapema kuwa safari hii hakuna kitakachomzuia kuchukua dola iwapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa kwa kumchagua ifikapo Oktoba 25.

Kiongozi huyo amekuwa na shauku kubwa ya kuongoza Wazanzibari kwa kuwa aliweka dhamira hiyo tangu alipoanza kusakamwa kisiasa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hata kufungwa gererzani bila ya kuhukumiwa kwa kosa lolote mahkamani.

Katikati ya mashaka ya kusakamwa na vyombo vya dola, Maalim Seif alipata kuapa kwamba “nitakuwa nanyi Wazanzibari nikiwa ndani au nje ya serikali.”

Safari hii amepata nguvu zaidi ya kupata ushindi baada ya kuwapata makada kutoka CCM waliojiunga kama hatua ya kuchoka utawala wa kidhalimu, akiwemo Mansour Yussuf Himid, aliyekuwa waziri katika serikali ya Amani Abeid Karume na hii ya Dk. Ali Mohamed Shein iliyoingia Novemba 2010, ambaye amemteua kuwa Katibu wa kamati maalum ya mkakati wa kumuingiza madarakani.

Wakati Maalim Seif amewateua Mazrui na Himid kuongoza kikosi cha kampeni kwa upande wa kisiwani Unguja, amempa kazi ya kuongoza kampeni kisiwani Pemba mwanasiasa makini injinia Othman Masoud Othman.

Masoud alikuwa waziri katika serikali ya pamoja, akajiuzulu katika uamuzi wa kuwajibika kutokana na ajali ya meli. Anagombea uwakilishi jimbo la kwao Ole, Pemba, wakati Himid anagombea jimbo jipya la Chukwani, Unguja.

error: Content is protected !!