August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Kinana mbumbumbu

Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Spread the love

MAALIM Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) amesema kwamba, Abdulrahman Kinana hajui chochote kuhusu kinachoendelea Zanzibar, anaandika Mwandishi Wetu.

Amesema Kinana ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM amekuwa akibeza juhudi za CUF kudia ushindi wake baada ya kuporwa na kutunukiwa Dk. Ali Mohamed Shein, rais wa Zanzibar.

Akizungumza kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kwenye Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar Maalim Seif ameonesha kumshangaa Kinana kwa kuzungumzia mgogoro wa Zanzibar akidai kiongozi huyo wa CCM hajui hatua zozote zilizofikiwa mpaka sasa.

Na kwamba, pamoja na Kinana kutojua mgogoro huo lakini hajui chochote kwenye nchi na hata ndani ya chama chake.

Pia Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais kupitia CUF visiwani humo mwaka 2015 amewataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu kwa kuwa, kimya kilichopo sasa kuhusu mgogoro huo kina mshindo mkubwa.

Amesema kuwa, suala la mgogoro wa Zanzibar linafanyiwa kazi na Jumuiya za Kimataifa na amewahakikishia kuwa juhudi hizo zitaleta matokeo mazuri.

Amewaambia Wazanzibari kwamba, yeye na chama chake waliporwa matokeo na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“…kimya kikuu kina mshindo mkubwa na wala msioni kama tumeshaachia,” amesema Maalim Seif na kuongeza “tunaendelea kupigania haki na haipo mbali In Shaa Allah.”

Pamoja na kuwepo kwa juhudi hizo Maalim Seif amewaambia Wazanzibari kwamba, kila kinachoendelea si vema kukiweka wazi kwa sasa kwa kuwa, wakati wake haujafika.

Kwenye kampeni hizo za kumnadi Abdulrazaq Khatibu Ramadhani, mgombea ubunge wa CUF, Maalim Seif ameongozana na Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na maofisa wengine wa vyma vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

 

 

error: Content is protected !!