January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Jeshi halitamaliza mgogoro Zanzibar

Spread the love

HUKU hali ya mambo hapa Zanzibar ikiwa haijatulia, Maalim Seif Shariff Hamad leo amesema mgogoro uliosukumwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha utatatuliwa kwa njia za kisiasa wala sio kiulinzi kama inavyojengwa taswira. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea)

Akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) Mtendeni mjini hapa, Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho na mgombea urais wa Zanzibar, amesema kuwepo kwa askari wengi wa vikosi mbalimbali nchini hakutasaidia kwa lolote kwani suala lililopo ni la kisiasa linalohitaji kutatuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Ni kweli unavyosema kuna maaskari wengi mitaani. Nami nashangaa lakini najua kwamba tuna tatizo la kisiasa linalopaswa kutatuliwa kisheria kwa kurudi kwenye msingi wa sheria na wala wananchiu wasidanganywe kuwa kuna njia nyingine,” amesema.

Maalim Seif alikuwa ameulizwa kwamba inakuaje anaendelea kuwapa matumaini wana-CUF na wananchi wa Zanzibar kuwa jitihada kubwa zinazofanywa na watu mbalimbali katika kutatua mgogoro uliotokea kuhusu matokeo ya uchaguzi kufutwa na Mwenyekiti Jecha, wakati ndani ya nchi wanaonekana maaskari wengi wakiwa na silaha nzito kama vifaru hadi kisiwa Pemba.

Amesema Rais Jakaya Kikwete ana dhamana ya kubeba katika hali iliyopo kwa kuwa ndiye pia Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Kwamba kama wananchi wanakuta maaskari wengi wenye silaha nzito, alisema, basi mtu hatakosea akisema na kuamini kuwa ni yeye Rais Kikwete anayeamrisha kuwepo kwa maaskari hao.

Akizungumzia jitihada zinazofanyika kutatua mgogoro, Maalim Seif alisema kwa kadri anavyojua, kuna matumaini makubwa ya kupatikana mafanikio ya jitihada hizo katika “Siku chache zijazo.” Alisema matatizo yaliyotokea yamesababishwa na kikundi kidogo tu cha watu wanaomsukuma Dk. Ali Mohamed Shein kwenda kwenye njia wanayoitaka wao ambayo aliita kuwa ni “inayojali maslahi yao binafsi wala si maslaha makubwa ya Wazanzibari.”

Maalim Seif amesema ameambiwa kwamba Mwenyekiti Jecha amerudi kazini na kuitisha kikao cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar huku akilazimisha kushawishi makamishna wa tume hiyo kumuunga mkono katika msimamo wake wa kuyafuta kinyemela matokeo ya uchaguzi akiwa ameshatangaza matokeo ya majimbo 32 kati ya 54 ya Zanzibar.

“Anahangaika bure huyu Jecha kwa sababu ameshindwa kutambua kwamba alichoota kukifanya ni kitu haramu kisichoungwa mkono na kifungu chochote cha Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya 1984 wala Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Msimamo wetu uko wazi kwamba tunataka Tume ifanye kazi yake, ikamilishe kuyatangaza matokeo ya kura zilizobaki na kumtangaza mshindi wa urais. Hapo itakuwa imewajibika,” alisema.

Maalim Seif amesema amekuwa akisisitiza kuwa uongozi atakaounda hautalipiza kisasi kwa mtu yeyote kwa sababu tayari siasa za kulipizana visasi zilishafutwa kufuatia kutandikwa kwa siasa za maridhiano zilizotokana na jitihada zake na Rais Mstaafu Amani Karume.

Katibu Mkuu wa CUF ambaye juzi aliweka muda wa saa 48 wa kutafutiwa ufumbuzi mgogoro wa uchaguzi uliotokana na uamuzi wa Mwenyekiti Jecha wa peke yake kufuta uchaguzi wote, amesema kwa kuwa anaridhika na jitihada zinazofanywa na kuutatua mgogoro, angali anaasa wananchi watulie na wasijihusishe na vitendo vya kuvunja sheria.

Mapema leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alitoa taarifa kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kwamba serikali inaunga mkono uamuzi wa Tume na kutaka wannchi watulie kusubiri hatua inayofata ya tume

error: Content is protected !!