July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Inaniuma kuhama CUF

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff

Spread the love

JEMEDARI wa siasa za upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza, hatua yake ya kuondoka katika Chama cha Wananchi (CUF) imeacha majonzi moyoni mwake. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Maalim Seif ambaye sasa ni mwanachama namba moja wa Chama cha ACT-Wazalendo, ameueleza umma kupitia kipindi cha 360 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds leo tarehe 1 Aprili 2019 kwamba, anaumizwa na hatua hiyo.

Amesema, ni sawa na mwanamume kumuacha mke aliyeishi naye muda mrefu na kuanzisha familia kwamba, kitendo hicho kinauma “lakini baadaye zitazoea na maumivu kuisha.”

Maalim Seif, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF ameeleza kuwa, kwenda kwake ACT-Wazalendo hakukuwa kitendo cha ghafla kwa kuwa, alisoma mazingira na kuaelewa.

“Hili jambo halikutokea kwa ghafla, lingetokea kwa ghafla ningeumia zaidi, tulishaona mwendo unavyokwenda.  Tuliona dola ina nia ya kumpa chama Prof. Lipumba (Prof. Ibrahim Lipumba), kwa hivyo katika kipindi chote tunavumilia.

“Tunasikia kuna mpango huu, sisi tukasema tusifanye haraka, kufikia wiki nne kabla tukaona maandishi yako ukutani na kwamba hakuna uwezekano wowote kwa sisi kupewa chama,” amesema Maalim Seif.

Amesema, baada ya kuwepo kwa viashiria vyote kwa Prof. Lipumba kukabidhiwa CUF, waliamua kuanza maandalizi ya kuondoka kwenye chama hicho.

“Kwa hivyo na sisi tukaanza kujitayarisha, ilivyotokea hata mtu ukimzoea nyumbani akaondoka ghafla unaumia, imekuwa sehemu ya maisha yako.

“Unaweza kuwa na mke ukaishi naye miaka 20 au 30, ukapata watoto na wajukuu, mwisho wa siku mke akaondoka, utaumia lakini baadaye utazoea tu,” amesema Maalim Seif.

Aidha amesema, uamuzi wa kujiunga na ACT haujavuruga wafuasi wake kwa kuwa, katiba ya chama hicho inafanana ya CUF na kwamba, hakuna matatizo lolote katika uamuzi wake.

“Sidhani kama tumewavuruga wananchama, sababu nao walichoshwa na walitaka mgogoro ufikie tamati, kwa hiyo mahakama ilipotoa uamuzi walioumua, baada ya saa tatu nilipotangaza kuhama ACT, wanachama walipata moyo mkubwa, na jinsi walivyohamasika, wameshukuru Mungu hili zigo limeondoka, sasa tunaangalia mambo mengine,” amesema Maalim Seif na kuongeza;

“Kuna mambo tulizingatia,  kuna vigezo tuliangalia, kwanza kuangalia Katiba vipi itashabihiana na Katiba ya CUF, sera hizi na tulizokuwa nazo na malengo ya CUF yanafanana au hayafanani. Tukaangalia chama kikoje kwa maana kwamba, kwenye uendeshaji wake, viongozi wake wako vipi, ni watu ambao unaweza kufanya nao kazi bila matatizo yoyote sababu tushachoka matatizo, usije kwenda pahala ukakutana na matatizo,” amesema.

Maalim Seif amesema, kilichotuvutia zaidi waliona ACT-Wazalendo ina uongozi vijana, bado wana nguvu. “Sisi wengine tunataka tuwape watu nafasi tuweze kufika, uongozi wenye malengo unajua unachotaka, wakishaamua lao wanalifanya na dhamira yao kwa nchi yetu ni nzuri.”

Amesema, yeye pamoja waliokuwa viongozi wa CUF wanashirikiana na uongozi wa ACT-Wazalendo katika kuleta mabadiliko ya kisiasa hapa nchini.

“Tupeni muda sababu tangu kujiunga ni kama wiki mbili, lakini mimi ninaamini kwa uongozi wa ACT ulivyo na uliotoka CUF ukaja pale,  mambo ambayo tutazingatia ni kwamba vipi tunaleta mabadiliko. Ni kweli lazima Watanzania waone mabadiliko, hilo tupeni muda na ndio dhumuni letu kwa sasa,” amesema Maalim Seif.

error: Content is protected !!