July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Hatutavumilia

Spread the love

MAALIM Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar ameanza kuitia kiwewe Zanzibar, anaandika Mwandishi Wetu.

Amesema, tabia ya mazombi visiwani humo kuendelea kushambulia wananchi hususan wanachama wa CUF haitavumiliwa tena kwa kuwa, wanaotesa wananchi hawachukuliwi hatua kali.

“Nasikitika kuona mazombi wakipiga wananchi na kuwajeruhi kila siku, pamoja na kuwepo kwa matukio haya waziwazi na polisi kuyaona lakini wanaendelea kuyakalia kimya,” Maalim Seif amesema na kuongeza kwamba “hali hiyo haitavumiliwa tena.”

Kutokana na kuendelea kwa mateso hayo kwa wananchi, Maalim Seif ameelekeza tuhuma zake kwa Jeshi la Polisi kutokana na kutochukua hatua dhidi ya mazombi.

Amelituhumu jeshi kwa kufanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya kulinda wananchi na mali zake.

Kauli hiyo aliitoa jana baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, visiwani Zanzibar akitokea India kwenye matibabu.

Visiwani humo, kumekuwepo na kundi la watu ambao hutumia magari yaliyo na usajili wa namba za serikali wakiwa wamejifunika sura zao na kuacha macho ambapo wamekuwa wakivamia baadhi ya Wazanzibari na kuwatesa.

Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF licha ya kuwa nje ya nchi, amekuwa akipata taarifa zote za kile kinachoendelea visiwani humo ikiwa ni pamoja na taarifa za vyombo vya habari zinazoandikwa kuhusu kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio Zanzibar.

Kuhusu Jeshi la Polisi Maalim Seifa amenukuliwa akisema “hapana shaka yoyote sasa limegeuka tawi la CCM.”

Malalamiko ya jeshi hilo kutumika na wanasiasa hususan CCM yamekuwa yakipaswa kutoka bara na viswani licha ya mara kwa mara kujinasua kwenye tuhuma hizo.

Mapokezi ya Maalim Seif yalihudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa CUF akiwemo Fatma Abdulhabibi Ferej, Nassor Ahmed Mazrui, Mansour Yussuf Himid na aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji.

Kwenye mapokezi hayo, alioneshwa kuridhishwa na namna viongozi wa CUF wanavyoendelea kusimamia msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio baada ya ule uliovurugwa na Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (CCM) kwa ushirikiano wa CCM.

Jecha ambaye ni mwanachama wa CCM aliyewahi kutafuta tiketi ya chama hicho kugombea ubunge Jimbo la Amani, Unguja katika Uchaguzi Mkuu 2010, alifuta uchaguzi huo kwa madai ya kuwepo kwa dosari licha ya kutokuwepo kwa chama chochote kilichowasilisha malalamiko hayo kwenye ofisi yake.

Hata hivyo, Maalim Seif alimtaja Dk. Ali Mohammed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwamba si miongoni mwa viongozi waungwana na wanaopaswa kupigiwa mfano kwa kuwa, amegoma kuondoka madarakani.

error: Content is protected !!