April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif, Mzee Moyo, wakinukisha Zanzibar

Viongozi wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar waliokuwa katika Kongamano la Maridhiano muda mfupi kabla halijavunjwa na Polisi

Spread the love

MAKAMU wa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, amemtuhumu Dk. Ali Mohamed Shein, rais wa sasa wa Zanzibar, kuwa anavivuruga visiwa hivyo. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea). 

Amedai, dhambi ya kuigawa Zanzibar na watu wake itaendelea kumuandama Dk. Shein, wakati taifa hilo ambalo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Dhambi ya kuigawa nchi hii haitafutika na Wazanzibari hawatakusamehe kwa hilo,” ameeleza Maalim Seif akimtaja Dk. Shein kuwa ameshindwa kuendeleza mfumo wa serikali ya maridhiano.

Amesema, Wazanzibari waliitaka serikali hiyo kwa kuuidhinisha kupitia kura ya maoni iliyopigwa tarehe 31 Julai 2010.

Alitoa kauli hiyo leo tarehe 31 Julai 2019, kwenye kongamano mahsusi la kuadhimisha miaka tisa ya kuasisiwa kwa mfumo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Kungamano hilo limefanyika kwenye ukumbi wa Baitul Yamin, visiwani hapa na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwemo viongozi mbalimbali wa kisiasa. Liliandaliwa na Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe nchini, Hassan Nassor Moyo.

Moyo ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi la kwanza la serikali iliyoongozwa na rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Maalim Seif alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika serikali ya kwanza chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) – Government of National Unity (GNU). Dk. Shein aliiongoza serikali hiyo kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Akionekana kukerwa na hatua ya Dk. Shein kuvuruga maridhiano, Maalim Seif alisema, “huyu Dk. Shein hajawatendea haki wananchi wa Unguja na Pemba, ambao waliamini mfumo waliouchagua wa uongozi wa kushirikisha vyama tofauti vya siasa, ndio unaowafaa kwa mazingira ya historia yao.”

Maalim Seif amesema, badala ya kuendeleza maridhiano ambayo msingi wake ni maafikiano ya tarehe 5 Novemba 2009, yaliyofikiwa kufuatia mazungumzo yake ya faragha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Abeid Karume, yeye Dk. Shein amekuja kuivuruga.

“Tulipokutana na Rais Amani Karume, tulikusudia kujenga siasa mpya za maridhiano ambapo watu wote watashiriki kuendeleza nchi yao… Tulikusudia kuondosha siasa za chuki na kubaguana. Hivi kama tungeendeleza pale, tungekuwa wapi leo,” alihoji.

Amesema, “nchi inaendeshwa kinyume na Katiba, kurekebisha sheria kwa dhamira ovu.” Amezitaja sheria zilizobadilishwa kwa nia ovu, kuwa ni pamoja na Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi.

Amesema matokeo ya kuvuruga mfumo wa maridhiano ni nchi kuendeshwa kibaguzi huku chuki zikitawala katika ajira; nafasi za masomo ya elimu ya juu na vyeo serikalini zikitolewa kwa upendeleo, jambo ambalo limezidisha ugumu kwa wananchi waliowengi.

Kwa mujibu wa Maalim Seif, chini ya uongozi wa Dk. Shein baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za miradi ya maendeleo, hasa inayogharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Amesema, chini ya uongozi wa Dk. Shein baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha ambako miradi mingi inayogharamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), ni ulaji wa wakubwa. Amedai kuwa baadhi ya vigogo kwenye serikali wamechukua mamilioni ya shilingi kutoka Benk ya Watu wa Zanzibar (PBZ).

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Mzee Moyo alisema, wazee kama yeye hawatakubali kuona Zanzibar inaongozwa kibaguzi na kwa chuki na kudharauliana.

“Haya ndio mambo ambayo yalikataliwa na kuondoshwa na Mapinduzi matakatifu ya 12 Januari 1964,” ameeleza Moyo na kuongeza, “Mzee Karume alitangaza kuwa ‘tumeshinda.’ Hakuna tena kutukanwa. Hakuna tena kudharauliwa. Hakuna tena kubaguana, maana sote ni Wazanzibari.”

Alisema, Mzee Karume alichagua viongozi wakiwemo waliokuwa wanachama wa Hizbu na baadaye Umma Party, kuingia kwenye serikali. Miongoni mwao, ni  Abdulrahman Mohamed Babu, Khamis Hemed na Salim Rashid ambaye alimteua kuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi.

“Huyu (Salim Ahmed Rashid), ni mwarabu aliyekuwa Hizbu na Umma Party. Ndiye aliyekuwa akichukua miniti za vikao vya BLM (Baraza la Mapinduzi). Nia ya Mzee Karume na shabaha yake ilikuwa ni kuunganisha watu bila ya kujali asili zao kwa maslahi ya Zanzibar,” ameeleza.

Amesema, “mimi ni Mngoni, lakini nimezaliwa hapa Zanzibar. Hututoki hapa. Maalim Seif hamnitoi, mimi mama yangu amezaliwa hapa. Na naipenda sana Zanzibar na watu wake. Tuache fitna na chuki, tuijenge nchi yetu.”

Naye mtaalamu mbobezi wa sheria nchini, Othman Masoud Othman ameeleza washiriki wa kongamano hilo kuwa mjadala juu ya hatima ya Zanzibar kisiasa na kijamii, ni jambo jema na muhimu sasa kwa lengo la kujenga mustakabali mwema wa nchi na vizazi vijavyo.

Othman aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar (AG) hadi mwaka 2014, amewaambia wananchi wa Zanzibar kujitambua wanapoendelea kutafakari hatima ya nchi yao na wasije wakachukua akili za maji ya togwa.

Alisema, “nawaasa wananchi wenzangu wa Zanzibar, msiwe maji ya togwa, kwa kuwa kwake juu ya mtama kwenye chupa yanajiona ndio bora kumbe sivyo… mtu akishika chupa ya togwa, huanza kwa kuitikisa ili apate ule mtama ambao ndio togwa.”

Maneno haya ya Othman yaliwachangamsha vya kutosha wananchi waliojazana kwenye ukumbi wa Baitul Yamini, mjini Zanzibar kuhudhuria kongamano maalum la kuadhimisha miaka tisa ya kuasisiwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.

Othuman alihutubia kongamano hilo, baada ya msemaji mkuu wa kongamano hilo, Maalim Seif Shariff Hamad, kumaliza kuzungumza.

Othman alisema, anayeitambua vizuri historia ya Zanzibar hawezi kujitambulisha katika namna inayoonesha kuwa yeye ndio Mzanzibari zaidi ya mwengine.

Alieleza asili ya togwa akisema kinywaji hicho cha asili visiwani Unguja na Pemba, ni mchanganyiko wa maji na mtama uliotengenezwa kwa kusagwa. Kwamba yale maji hujiona ni bora zaidi kwa kuwa yanaonekana juu pale chupa inapokuwa imetulia.

“Lakini mtu anapoikamata chupa ya togwa, ni lazima aanze kwa kuitikisa. Anafanya hivi kwa sababu shida yake siyo yale maji bali anataka mtama ambao ndio wenye rutuba mwilini mwake. Kwa mnywaji huu mtama ndio togwa si maji,” alisema.

Alichangamsha ukumbi kwa simulizi hiyo aliyoitoa kama nasaha zake kwa Wazanzibari baada ya kuwa ameeleza ukweli wa historia yao akisema hata Jeshi la Polisi la Zanzibar baada ya Mapinduzi, lilikuwa na wananchi 200 tu wa asili ya Zanzibar huku wengine waliobaki wakiwa ni watu waliokuwa na asili ya Tanganyika, Kenya, Malawi na Uganda.

Alisema mshikamano na umoja kwa Wazanzibari ndio jambo pekee litakalowafikisha kwenye nchi nzuri inayoweza kupiga hatua ya maendeleo na ikajivunia kwayo.

Alisema si wengi wanaojua kuwa mji wa Chake Chake, kisiwani Pemba, kwa sehemu kubwa umejengwa kwenye shamba la Nassor bin Khelef aliyekuwa akiishi hapo; ujenzi ulianza kwa nyumba 200 hivi katika mwaka 1908.

Wakitokea wajukuu na vitukuu vyake bin Khelef kutaka kumiliki shamba hilo, inakuwa ni haki yao ambapo wale wasiojua watapinga kwa udhaifu wao wa kutojua au kuamini katika ubaguzi wa asili za watu.

Othman amemwagia sifa Maalim Seif kwa kusema, ni kiongozi mwenye hekima kubwa ambaye kuwepo kwake, ni tunu muhimu kwa Wazanzibari.

“Huyu Maalim Seif ni mtu mwenye hekima kubwa sana kusema kweli. Tuna bahati kubwa sisi. Amekuwa akizuia farka hapa Zanzibar lakini wapo wanaodharau ukweli huu wa historia,” alieleza Othuman kwa sauti ya msisitizo.

Othman alieleza umuhimu wa kuhimiza umoja na mshikamano katika Zanzibar kwa kuwa ni jambo jema lililotajwa ndani ya kitabu kitukufu cha Quran kupitia Surat Bakra, kuanzia aya ya 269.

Akasema inasikitisha kuendelea kwa mipango ya wasioipenda Zanzibar kuwa ya mshikamano akiwanasibisha na fisi, ambaye anatamani mkono wa binadamu uanguke ili apate chakula. Watu hawa si hasha wanamdharau Maalim Seif kwa sababu anazuia Zanzibar kugeuzwa Creamea, nchi inayotwaliwa kimabavu na Russia baada ya kuitenganisha na Ukraine.

Anasema, nchi zote zilikuwa zilikuwa zimeungana katika Umoja wa Kisovieti wa Urusi (USSR) uliokuja kuvunjika kufuatia sera za Mikhail Gorbachev kwenye miaka ya mwanzo ya 1990.

“Kwa yale aliyoyaeleza Maalim Seif mimi siwezi kuyakiuka maana namheshimu sana Maalim Seif ndio muasisi khasa wa maridhiano yaliyoiweka Zanzibar kuwa nchi ya watu walioshikamana na kushirikiana kuijenga pamoja,” alisema.

Othman alitoa simulizi nyengine ya utata wa pundamilia ambaye watu wanatofautiana kusema ni mnyama mweupe mwenye mistari myeusi au ni kinyume chake.

Kongamano hilo lilisimamishwa saa sita mchana kwa agizo la Jeshi la Polisi. Hata hivyo, baadaye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka, alinukuliwa akisema, jeshi hilo hawakuvunja kongamano; isipokuwa muda wake ulikuwa umekwisha na walioandaa waliamua kulisitisha.

error: Content is protected !!