November 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif ‘byebye’ CUF

Spread the love

JINA la Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) linakwenda ukingoni ndani ya chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Hatua hiyo inakuja baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa kanda na kupata wajumbe wa Baraza la Uongozi wa CUF ambapo leo tarehe 16 Machi 2019 litajadili na kupitisha jina la Katibu Mkuu mpya wa chama hicho kati ya majina matatu yatakayoteuliwa na mwenyekiti wa chama hicho.

Kwa mujibu wa mabadiliko madogo yaliyofanywa katika Katiba ya CUF, mwenyekiti atateua majina matatu kwa kushirikiana na makamu mwenyekiti bara na visiwani.

Kisha majina hayo atayawasilisha katika Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho ambalo litaketi leo ili kupitisha jina moja la Katibu Mkuu.

Kufanyika kwa hatua hiyo, kunatoa tafsiri kwamba, Maalim Seif ambaye ndiye Katibu Mkuu wa sasa, nafasi yake itakuwa imefika ukingoni. Kutokana na utaratibu huo, jina la Katibu Mkuu wa CUF linaweza kupatikana kati ya leo ama kesho tarehe 17 Machi 2019.

Abdul Kambaya, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma CUF akizungumza na MwanaHALISI ONLINE amesema, utaratibu huo ndio utatumika kumpata Katibu Mkuu mpya wa CUF kati ya leo na kesho.

“Mwenyekiti atateua majina matatu na hapo Baraza Kuu la Uongozi litachagua jina moja na hivyo utaratibu utakuwa umekamilika na kumpata Katibu Mkuu wa chama,” amesema.

Tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeeleza kuwa, mikutano inayofanya na CUF kwa upande wa Prof. Lipumba inatambulika na kwamba, imefuata katiba ya chama hicho.

Kwenye mkutano wa Baraza Kuu ulioanza tarehe 12 Machi 2019, Sisty Nyahoza, Naibu Msajili aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba, unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya CUF na kwamba, ndio maana amefika kuwakilisha Ofisi ya Msajili.

Kwenye mkutano huo Nyahoza amewapongeza CUF Lipumba kwa kufanikiwa kusajili Bodi ya Wadhamini pamoja na kuhimili mikiki ya mahakama kwa dhamira ya kulinda chama hicho.

Kumekuwepo na mgogoro kati ya Rrof. Lipumba na Maalim Seif na kusababisha wanachama wa chama hicho kupasuka vipande viwili. Mgogoro huo ulianza pale tu Prof. Lipumba alipotaka kurejea madarakani baada ya kujiuzulu.

Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa CUF kwa hiari, tarehe 6 Agosti 2015, kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa maelezo kuwa, amekosa ushirikiano na viongozi wenzake.

Alisema, kwa namna chama kinavyokwenda, nafsi yake inamsuta kuendelea kuwa kiongozi. Akatangaza kung’atuka na kudai kuwa atabakia kuwa mwanachama muaminifu na iwapo chama kitaridhia anaweza kuwa mshauri wake.

Prof. Lipumba alishikilia uamuzi wake wa kujiuzulu licha ya kuombwa kutofanya hivyo na viongozi wenzake wa juu akiwemo Maalim Seif. Kurejea kwake kumevuruga chama hicho ambapo kesi mbalimbali zimefunguliwa dhidi yake na wale wanaomuunga mkono ndani ya chama hicho.

error: Content is protected !!