July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif azushiwa kifo

Spread the love

MAALIM Seif Sharif Hamadi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) amezushiwa kifo. Baadhi ya mitandao ya kijamii nchini imeripoti taarifa hiyo, anaandika Hapyyness Lidwino.

Taarifa hizo zimeendelea kusambaa kwa kasi ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi huyo wa CUF kupelekwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, kupatiwa matibabu mara tu baada ya kushuka kwenye ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Mtandao huu umemtafuta Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Umma wa CUF ili kupata ufafanuzi wa taarifa hizo bila mafanikio.

Hata hivyo Sheweji Mketo, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF ameuambia mtandao huu kwamba, habari hizo ni za uzushi na hazina ukweli wowote.

“Kweli nimesikia na kusoma kutoka kwenye mitandao mbalimbali kwamba eti Maalim Seif amefariki. Kwa hakika taarifa hizo ni za uzushi kabisa.

“Maalim Seif yupo salama, habari zinazoenea zina lengo lingine kabisa. Anaendelea vizuri na hana ugonjwa wowote kama ambavyo imekuwa ikielezwa kwenye baadhi ya taarifa na nimezungumza naye mchana huu,” amesema Mketo.

Amefafanua kwamba, sababu ya Maalim Seif kupelekwa Hindu Mandal jana ni baada ya kujisikia kizunguzungu mara tu baada ya kushuka kwenye ndege kutokana na uchovu wa safari.

Amesema, baada ya hali hiyo, wataalamu wake wa masuala ya afya walimshauri aende kupumzika huku akiangaliwa zaidi afya yake.

“Afya yake imeimarika na tayari ameshatoka kesho anatarajia kuendelea na ratiba zake kama kawaida.hata mchana huu alikuwa anaongea na waandishi wakati akiwa hospital, amesema mketo,” amesema Mketo.

Hivi karibuni, Maalim Seif amerejea kutoka India alipofanyiwa matibabu ya mgongo ambapo jana alikwenda Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za kichama na kukutwa na mkasa huo.

error: Content is protected !!