January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif: Askari, wanajeshi acheni kutumiwa na CCM

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff

Spread the love

VIKOSI vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimetakiwa kuacha kutumiwa kisiasa na kwenda kinyume na sheria zinazoongoza kazi zao. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Hamad amesema “Kutumiwa Kambi ya JWTZ iliyopo Chukwani, kisiwani Unguja kuandikisha mamia ya vijana ambao si wazanzibari na kuwapatia Vitambulisho vya Mzanzibari (ZAN IDs) kwa ajili ya kuja kuandikishwa kama wapiga kura ni kuvunja sharia”.

Hamadi amesema tayari vijana 20,000 wameandikishwa na kupewa ZAN IDs. Vijana 700 walichukuliwa katika maeneo mbali mbali ya jimbo la Uzini na ambao wamepelekwa kusajiliwa katika jimbo la Bububu kisiwani Unguja.

“Vijana wapatao 10,000 waliohamishwa kutoka Wilaya ya Kati Unguja na kusajiliwa katika majimbo ya Dimani na Mtoni katika Wilaya ya Magharibi Unguja na majimbo ya Chumbuni na Kwamtipura katika Wilaya ya Mjini Unguja.

“Pia kuna vijana 1,200 wamepatiwa ZAN IDs kwa ajili ya kuja kuandikishwa katika jimbo la Chonga na wengine 1,000 katika jimbo la Mkanyageni, kisiwani Pemba,” amesema Hamadi.

Aidha, amesema katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wengi wao wakiwa baina ya miaka 14 hadi 17 wamekuwa wakichukuliwa na kupelekwa kituo cha kusajili vitambulisho vya Mzanzibari kilichopo Gamba ambako wamepatiwa ZAN IDs na sasa wanasubiri kuandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura.

Mbali na uvunjwaji sharia katika uandikishwaji, pia ucheleweshaji wa ugawaji wa majimbo ya uchaguzi chini ya usimamizi wa Sekretarieti ya ZEC imekuwa ni kero.

“Tunazo taarifa za kuaminika kabisa kwamba Tume ilikwisha kamilisha kazi hiyo kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wananchi na ripoti ya mapendekezo kutayarishwa.

“Kwa sababu mapendekezo hayo hayakukiridhidha CCM, yaliwekwa upande na sasa CCM imeitumia Wizara ya Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuandaa mapendekezo mengine ambayo yameandaliwa kwa lengo la kupunguza majimbo katika maeneo yenye wafuasi wengi wa CUF na kuongeza majimbo kwenye maeneo yenye wafuasi wengi wa CCM,” ameongeza Hamad.

Hamadi amesema ili kuiepusha nchi na vurugu zinazoweza kutokea kwa kukiuka misingi ya katiba na sheria katika uendeshaji wa uchaguzi huru ni lazima: Wapiga kura haramu wote waliopatiwa vitambulisho vya Mzanzibari kinyume na sheria watakiwe kuvisalimisha na wasiandikishwe katika Daftari la Wapiga Kura.

Aidha, watu wote wenye haki ya kupatiwa ZAN IDs wapewe vitambulisho vyao kabla ya uandikishaji wa mwisho unaotarajiwa kuanza tarhe 16 Mei mwaka huu ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba kujiandikisha na kupiga kura.

Vikosi vya Ulinzi na Usalama vikiwemo JWTZ na Idara Maalum za SMZ ziache kutumiwa kisiasa na kwenda kinyume na sheria zinazoongoza kazi zao ambazo zinakataza kujiingiza katika masuala ya kisiasa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ) aache kuwatumia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha katika kusajili wapiga kura haramu kwa kuwapatia ZAN IDs na wakati huo huo kuwakatalia wapiga kura halali haki ya kusajiliwa na kupatiwa ZAN IDs.

Idara ya Usajili wa Wazanzibari iache kutumika kisiasa kwa kusajili watu wasio Wazanzibari, watoto wadogo na watu wanaotoka nje ya majimbo yao kwa lengo tu la kukisaidia CCM, Jeshi la Polisi lisikubali kutumiwa kinyume na sheria kuwalinda wapiga kura hao haramu wanapopelekwa kwenda kujiandikisha.

Daftari la Wapiga Kura lifanyiwe uhakiki kwa mfumo wa kielektroniki unaotumia bio-metric features ili kuwafuta waliosajiliwa zaidi ya mara moja na pia kuwaondoa waliofariki na watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

error: Content is protected !!