April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Makamu wa Kwanza wa Rais Z’bar, ‘mweupeee’

Maalim Seif Shariff Hamad

Spread the love

MAKAMO wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seiff Sharif Hamad, hana mamlaka ya “kutumbua, kuteua; na au kushika kiti cha urais, ikiwa rais aliyeko madarakani, hayupo katika kiti chake. Anaripoti Brightnes Boaz, Dar es Salam … (endelea).

Maalim Seif aliapishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussen Mwinyi, kushika nafasi wadhifa huo, Jumanne iliyopita, tarehe 8 Desemba 2020, Ikulu mjini Unguja.

Ameapishwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais, kupitia wajibu uliotajwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010.

Maalim Seif, ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar, kupitia ACT-Wazalendo, katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020, hii imekuwa mara yake ya pili kushika nafasi hiyo.

Aliwahi kuhudumu katika wadhifa huo, mwaka 2010 hadi 2015, kipindi cha utawala wa Dk. Ali Mohamed Shein, wakati huo alikuwa Chama Cha Wananchi (CUF).

Katiba ya Zanzibar, inaelekeza kuwapo Makamo wawili wa Rais – Makamo wa kwanza na yule ya pili – na kusema, “Makamo wa Kwanza wa Rais atatokana na chama kilichoshika nafasi ya pili kikiwa na zaidi ya asilimia kumi ya kura zilizopatikana kwenye uchaguzi mkuu wa rais.”

Kwa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais, Katiba inaeleza, atateuliwa na rais kutoka chama ambacho rais huyo aligombea na kutangazwa kuwa mshindi.

Kwa matokeo yalivyotangazwa na Tume ya taifa ya uchaguzi Zanzibar (ZEC), Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilishinda uchaguzi huo na ACT-Wazalendo kilishika nafasi ya pili, hatua ambayo imewapa nafasi ya kuingia serikalini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais ndiye mwenye mamlaka makubwa, kulinganisna na makamo wa kwanza, ikiwamo kuwa Kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi na kuwa na uwezo wa kushika nafasi ya urais, pale rais aliyepo madarakani anapokuwa hayuko ofisini.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Kwa mujibu wa Katiba, Makamu wa Kwanza wa Rais, hataruhusiwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Badala yake, ametajwa kuwa “atakuwa mshauri mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake na atafanya kazi zote atakazopangiwa na rais.”

Aidha, Makamo wa Kwanza wa Rais, hataruhusiwa kushika madaraka ya Rais iwapo Rais aliyepo madarakani atakuwa yuko nje ya nchi, au kukutwa na jambo jingine lolote ambalo litamfanya kupoteza sifa ya kuwa rais.

Kifungu cha 39 (1) cha Katiba ya Zanzibar, kinasema, pamoja na kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais na yule wa Pili, “wakati wote watakapokuwa madarakani watawajibika kwa Rais,” lakini “Makamu wa Kwanza wa Rais, haruhusiwi kushikilia nafasi ya Rais hata kwa dakika moja, pale rais aliyepo madarakani anapokuwa hayupo kwenye kiti chake; na au amesafiri nje ya nchi.”

Ibara ya 33 (1) ya Katiba inasema, “endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kwa kufariki; au kujiuzulu; au maradhi ya kimwili au kiakili; au sababu nyengine yoyote ikiwamo Rais kuondoka nchini au kutoweza kutekeleza kazi zake, watu wafuatao, kwa mujibu wa mpangilio, watashika nafasi hiyo:

“Makamu wa Pili wa Rais, au ikiwa hayupo; Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye anatoka katika chama anachotoka Rais na yeye ikiwa hayupo, nafasi hiyo itashikiliwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar.”

Katiba ya Zanzibar, haijaeleza kokote mamlaka ya Kiongozi huyo wa Pili baada ya rais – Makamo wa Kwanza wa Rais – ya kutengua, kuteuwa, kuwajibisha, kusimamia, kutoa maagizo, zaidi ya kusimamia maamuzi ya pamoja ya Baraza la Mawaziri.

Badala yake, Katiba inamtaka Makamo wa Kwanza wa Rais kuwa atashauriana na Rais kuteua Naibu Mawaziri kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kumsaidia Rais.

Katiba ya Zanzibar inampa mamlaka Rais kumfuta kazi makamo wake na baadaye kukitaarifu chama chake, kupendekeza kwake, jina la mtu mwingine ili kushika nafasi hiyo.

Katiba inasema, “iwapo mtu atafutwa katika nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais kwa mujibu wa kijifungu cha (1)(b) cha kifungu hiki, chama chake si zaidi ya siku kumi na nne kinatakiwa kupendekeza kwa Rais jina la mtu mwengine.”

Mbali na mamlaka ya rais ya kumfuta kazi makamo wake, Ibara ya 41.(1) inaeleza kuwa Baraza la Wawakilishi linaweza kupitisha Azimio la kura ya kutokuwa na imani na Makamo wa Kwanza wa Rais au Makamo wa Pili wa Rais endapo itatolewa hoja kupendekeza na ikapitishwa na theluthi mbili ya wajumbe wake.

Kwa sasa, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, linaongozwa na CCM kwa zaidi ya asilimia 90 ya wajumbe wake.

error: Content is protected !!