August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif amvuruga Dk. Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Spread the love

NI wazi sasa Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar anavurugwa na harakati zinazofanywa na Maalim Seif Sharif ndani na nje ya Zanzibar, anaandika Mwandishi Wetu.

Akizindua Soko na Ofisi ya Baraza la Maji la Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba jana ikiwa ni kuelekea Sherehe za Miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar Dk. Shein alitupa kijembe kwamba, hakuna rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo.

Na kwamba, kumekuwepo na wapinzani ambao wanatamba na kujinadi mitaani kuwa, wanaweza kuwa rais wakati wowote huku wakidai yeye si rais halali visiwani humo. Dk. Shein amewataka wananchi kupuuza kauli hizo.

Dk. Shein hakutaja jina la anayemtuhumu kujinadi kwamba atakuwa rais muda wowote lakini anayekusudiwa hapo ni Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na aliyegombea urais visiwani humo kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Maalim Seif amekuwa akitamba kwamba, ataishinda Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk. Shein kutokana na kupora ushindi wake kwenye uchaguzi wa mwaka juzi.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilifuta uchaguzi wa awali kinyume na Katiba ya Zanzibar na kuitisha uchaguzi mwingine tarehe 20 Machi mwaka jana ambapo baadhi ya vyama kikikwemo CUF vilisusia uchaguzi huo.

Kwenye uchaguzi wa awali CUF ilidai kushinda na kwamba, Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC alivuruga uchaguzi huo kutokana na mahaba yake kwa CCM.

Maalim Seif amekuwa akiwaambia Wazanzibari kwamba, haki yake ya kuwa rais inakaribua kutimia na kwamba, Dk. Shein sio rais halali wa Zanzibar.

Tayari Maalim Seif amefikisha suala la kuporwa haki yake ya urais visiwani humo katika Jumuiya za Kimataifa huku akisema, mwelekeo ni mzuri.

Siku za karibuni Maalim Seif alinukuliwa akisema “hata wafanye kitu gani, mwaka huu msumari umewaganda na hivi karibuni Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.”

Akifungua uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo kwenye Jimbo la Dimani, Maalim Seif alimshambulia Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM kuwa, hajui chochote kinachoendelea kuhusu mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

Alifanya hivyo kwa madai kwamba, Kinana amekuwa akibeza juhudi za CUF kudia ushindi wake baada ya kuporwa na kisha ZEC kumtunuku Dk. Shein.

Maalim Seif ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2010-2015 aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu kwa kuwa, kimya kilichopo sasa kuhusu mgogoro huo kina mshindo mkubwa.

“…kimya kikuu kina mshindo mkubwa na wala msioni kama tumeshaachia,” alisema Maalim Seif na kuongeza; “tunaendelea kupigania haki na haipo mbali In Shaa Allah.”

Kwenye kampeni hizo za ubunge alikuwa akimnadi Abdulrazaq Khatibu Ramadhani, mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CUF.

error: Content is protected !!