January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif amuinua Lowassa Z’bar

Spread the love

KAMPENI ya Maalim Seif Shariff Hamad ya kushika madaraka ya Zanzibar imeanza kwa nguvu kwa kupata ugeni mzito wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Edward Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Maalim Seif, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye katika serikali inayomaliza muda mwezi ujao ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais, alizindua kampeni yake jioni hii kwenye uwanja wa Kibandamaiti, mjini Zanzibar.

Mkutano huo, ulishuhudiwa na Lowassa, kada aliyehama CCM mwezi uliopita, na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kuteuliwa kuwania urais kwa mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Lowassa alitumia dakika chache kuwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa wapige kura kwa amani na utulivu na “hakuna atakayeziiba kura zao.”

“Hawawezi kutuibia, msiogope kitu… tuna uwezo wa kulinda kura zetu. Huo uwezo tunao, au mnadhani hatuna,” amesema na kuambiwa “tunao.” Alijibu vilio vya hofu ya kutokea wizi wa kura kama ambavyo Zanzibar imekuwa ikishuhudiwa kila uchaguzi.

Lowassa ametoa wasiwasi umma na vitisho kuwa chama cha upinzani kikishinda, kutakuwa na vurugu, akisema hakutakuwa na vurugu yoyote. “Vurugu zitoke wapi, kwani hapa kuna vurugu iko wapi na tumekutana hapa kwa wingi,” amesema Lowassa huku wananchi wakimshangilia.

Ameahidi kuwa baada ya ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 25, ataomba sehemu ya sherehe ifanyike mjini Zanzibar, kwa kuwa pia “itakuwa ni sherehe kwa ushindi wa Maalim Seif.” Aliomba wananchi wampigie kura nyingi yeye pamoja na Maalima Seif ili waunde serikali makini pande zote mbili.

Lowassa amelaumu kitendo cha wapinzani wake kuchukua mabango ya picha zake na kuyaharibu. “Wanachukua mabango yetu wameyaangusha. Tumewaambia tutafanya kampeni za kistaarabu lakini angalia wanavyofanya,” amesema.

Akihutubia umma uliohudhuria mkutano huo baada ya uteuzi wa wagombea urais kufanywa jana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Maalim Seif alisema akishika madaraka, atawarudisha masheikh Zanzibar.

“Nikiwa rais masheikh wetu watarudi Zanzibar, kama wana makosa watashitakiwa katika mahakama zetu ambazo ziko sawa na Mahakama ya Tanzania Bara,” amesema.

Awali alisema inashangaza kuambiwa Zannzibar ina rais, ina Baraza la Wawakilishi na ina Mahkama, ambayo mamlaka yake sawa na mahkama ya Bara, lakini “waliamua masheikh wetu kuwapeleka Bara, nasema watarudi haraka mara tu nikiwa rais.”

Maalim Seif ambaye anagombea mara ya tano ndani ya malalamiko ya kuporwa ushindi wake, amesema amejiandaa kuibadilisha Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki kwa kiwango cha maendeleo.

  • Nia yangu ipo palepale ya kuibadilisha Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika Mashariki kwa maendeleo makubwa. Tutaijenga Bandari ya Zanzibar kwa vitendo sio maneno, tutafungua uwanja wetu mpya wa ndege na kuhakikisha unakuwa na eneo la mizigo mikubwa ili Burundi, Rwanda, Zambia waje kununua bidhaa hapa.
  • Tutaungua Benki ya Uwekezaji ya Zanzibar ya kutoa mikopo kwa wanawake na vijana wenye shida ya mitaji ya kufanyia biashara zikiwemo za Jua Kali.

Maalim Seif amesema serikali atakayoongoza itakuwa na utii kwa utawala wa sheria na haki za binadamu na kamwe haitaruhusu watu kudhalilishwa na askari wa vikosi kama inavyofanyika askari wanaojifunika nyuso na kutesa wananchi.

error: Content is protected !!