August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif amtia kiwewe Dk. Shein

Spread the love

KIWEWE cha Serikali ya Dk. Ali Mohammed Shein kinakomaa, matokea ya kukanyagwa demokrasia visiwani Zanzibar yanatesa utawala wake, anaandika Faki Sosi.

Kutokana na Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa mgombea urais visiwani humo kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kuinyima usingizi Serikali ya Dk. Shein, kumekuwepo na mikakati ya kuhakikisha anadhibitiwa haraka.

Juzi Jeshi la Polisi limemuhoji Maalim Seif visiwani humo ikiwa ni siku moja kupita baada ya Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Zanzibar kutoa taarifa ya jeshi hili kushinikizwa na CCM kufanya hivyo.

Hamdan Makame, Kamishna wa Polisi Zanzibar alikiri kwamba, kiongozi huyo wa CUF amehojiwa na jeshi hilo bila kutaja jambo ambalo lililisukuma jeshi hilo kumuhoji.

Taarifa kutoka ndani ya CCM zinaeleza kwamba, kinacholengwa na Serikali ya Dk. Shein ni kumdhalilisha Maalim Seif kwa wananchi.

“Hii inafanywa kwa kusudi maalum, si kwamba serikali haijui isipokuwa ni kutaka kumdhalilisha na kumsumbua ili achoke na kazi ya siasa.

“Ni kweli kwamba serikali ya bosi (Dk. Shein) ni kama haina nguvu vile, nina maana inatawala wafanyakazi wa serikali na si wananchi. Wananchi wana hasira hasa wanapobaini maamuzi yanatoka Bara na serikali ya huku inatekeleza tu. Hata sisi ndani ya chama hiko kinatukera,” amesema mtoa taarifa ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Miongoni mwa mambo yanayosimamiwa na Maalim Seif na yanayosababisha athari kubwa katika utawala wa Dk Shein ni kuwataka wanachama na wapenda haki visiwani humo kujitenga na utawala huo ambao (Maalim Seif) anautaja kuwa haramu.

Msimamo huo umepokewa na kutekelezwa na wanachama hao na kimesababisha Dk. Shein kuyumba.

Tayari chuki za kisiasa zimeshamiri visiwani humo ambapo wananchi hao amekuwa hawauziani bidhaa kutokana na itikadi za vyama vyao.

Awali Mazrui alisema, sababu ya polisi kumsaka Maalim Seif ni kudaiwa kufanya maandamano alipokuwa Pemba na kwamba, kiongozi huyo wa wa CUF hakulifanya.

Katika taarifa ya Mazrui juzi alisema, si Maalim Seif pekee, viongozi wengine wa chama hicho wanaoundiwa mkakati wa kukamatwa ni pamoja na Mansoor Yussuf Himid na Nohamed Ahmed Sultan kwa sababu za kisiasa.

“Tunazo taarifa kwamba, kuna wanasiasa wameliagiza Jeshi la Polisi kuandaa mashtaka kwa ajili ya kumshitaki Maalim Seif Sharif Hamad kwamba, alipokuwa Pemba alifanya maandamano bila ya kibali wakati hakukuwa na maandamano yoyote.” Alisema na kuongeza;

“Viongozi hao wamepangiwa kukamatwa na kuletwa katika magereza ya Tanzania Bara kwa lengo la kuwanyamazisha Wazanzibari ili wasipaze sauti zao kupinga utawala wa kidikteta uliowekwa madarakani kwa nguvu za dola kinyume na matakwa ya kidemokrasia ya wananchi wa Zanzibar.”

Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF ameueleza mtandao huu kwamba, kinachofanyika sasa ni matokeo ya msimamo wa chama hicho dhidi ya Serikali ya CCM Zanzibar.

“Serikali ya Dk. Shein inateseka, tulisema tutadai haki kwa njia ya amani na hii ndio inawatesa zaidi. Wazanzibari hawakumtaka Shein, CCM wakamtaka na sasa Wazanzibari wamemwacha Shein aongozi wana-CCM pekee.

“Kumsumbua katibu mkuu wetu hakutarudisha nyuma harakati hizi. Tunachoridhika ni kwamba Wazanzibari wanaonesha kwa vitendo kumkataa Shein na hili ndio linawauma zaidi. Shein hakushinda, alipewa urais na yeye anajua hilo,” amesema Kambaya.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi halali visiwani Zanzibar 2015, visiwa hivyo vimeingia katika sintofahamu.

Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema amesema kuwa, CCM inashindwa kujifunza kwa yale yaliyotokea miaka ya nyuma na kwamba, kinachofanywa na Serikali ya Dk. Shein hakina matokeo yoyote hasi kwa Maalim Seif.

Amesema Serikali ya CCM imeiba kura za CUF kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana lakini haijatosheka na sasa wanaendeleza mabavu kutaka kuwanyamazisha wapinzani.

Amesema kuwa, Maalim Seif licha ya kukamatwa na kuwekwa kuzuizini mwaka 198 hadi 1991 chini ya utawala wa Mwalim Julius Nyerere, hakukupunguza kasi yake.

Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana unatajwa kumpa ushindi Malim Seif ambao ulipokwa na kada wa CCM ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha na kisha kumtunuku Dk. Shein baada ya kulazimisha uchaguzi wa marudio kinyume na katiba ya Zanzibar uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

error: Content is protected !!