January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif ampopoa Prof. Lipumba

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amebeza kauli ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba kwamba, wapinzani wamepoteza mwelekeo wa kupata katiba ya wananchi. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Amesema, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vitasimama imara kutetea maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaaf, Joseph Warioba.

Wakati akitangaza kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba alisema, watu waliopinga mapendekezo ya Katiba ya Wananchi ndio wanaohamia upinzani na kwamba, hatua hiyo itasababisha kushindwa kupatikana kwa katiba iliyo na maoni ya wananchi.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi wa UKAWA katika Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Maalim seif amesema, dhamira ya umoja huo ni kupigania maoni ya wananchi na si yale yaliyopitishwa na CCM.

Kinyume na alivyoeleza Prof. Lipumba kuwa, umoja huo umepoteza dira katika kupigania maoni ya wananchi, Maalim Seif amesema, timu iliyopo inatosha kurejesha maoni ya wananchi yatakayowezesha kutunga Katiba Mpya.

“Nawahakikishia kuwa, mimi na Duni Haji (mgombea mwenza wa Chadema) pamoja na mgombea urais (Chadema), Edward Lowassa tutarejesha katiba iliyo na maoni ya wananchi,” amesema Maalim Seif.

Pia amesmea, Katiba iliyopitishwa na CCM bungeni ilipinduliwa na haikubeba maoni ya wananchi isipokuwa maoni ya CCM.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa UKAWA, Maalim Seif amesema, CCM wamekuwa wakieneza propaganda kwamba, ana dhamira ya kuvunja muungano. Hata hivyo amesema;

“Nawahakikishieni kwamba, dhamira yangu si kuvunja muungano isipokuwa kuwepo na muungano ulio na maslahi kwa wote,” amesema na kuongeza; “nawaulizeni, nani aliwahi kunisikia kuwa nataka kuvunja muungano?” hata hivyo wanachama wake walijibu “hakunaaa.”

Hata hivyo, Maalim Seif alimwambia Lowassa kuwa, walioandamana kwenye msafara wake wa kwenda kuchukua fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) ni vijana.

“Wengi waliokusindikiza leo ni vijana, hawa wana matumaini na wewe ubadilishe maisha yao, walikuwa wameishakata tamaa na hawana imani tena na serikali iliyopo. Hawa wana imani na wewe,” amesemea.

Amesema kuwa, Lowassa ni muungwana “ukiaminiwa na utekeleze” na kuwa, vijana hao wanataka kuondokana na umasikini kutokana na nchi yao kuwa na utajiri mkubwa.

“Tutaiondoa CCM si kwa maandamano, tutaiondoa CCM kwa kupiga kura,” amesema Maalim Seif na kuongeza kuwa, wanapaswa kujitokeza wakati wa kupiga kura kwa lengo moja “kuing’oa CCM madarakani.”

error: Content is protected !!