January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif amfuata Balozi Seif Kitope

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad

Spread the love

WAKATI Balozi Seif Ali Idi akisema hampendi Maalim Seif Shariff Hamad, viongozi wasaidizi wakuu wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kesho Maalim anatarajiwa kuhutubia jimbo la Kitope, ambako watu wapatao 600 watapokea kadi za uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), wakiitenga CCM. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Hii ni hatua ambayo wanajimbo wenyewe wameitaka. Wamefikisha maombi kwa uongozi wa juu wa CUF kutaka Maalim Seif, afike kuwahutubia akitangulia na kukabidhi kadi za uanachama wa CUF kwa kuwa wanaamini si haki yao kubakia CCM.

Na hatua hii inakuja miaka miwili baada ya Maalim Seif kufika jimbo hilo analoliwakilisha Balozi Seif katika Bunge la Jamhuri ya Muungano, na kukabidhi kadi kwa watu wapatao 500, idadi kubwa wakiwa ni vijana.

Alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika uwanja wa mpira, Upenja, Maalim Seif aliwahakikishia vijana kupata fursa za ajira atakapokuwa anaongoza serikali baada ya uchaguzi, hasa kwa kuwa atatekeleza sera za kiuchumi zitakazoifanya Zanzibar eneo kivutio cha biashara ndani ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Alisema Zanzibar itakuwa Dubai katika kanda hii, sera ambayo itanufaisha kundi kubwa la vijana wasiokuwa na ajira hata baada ya kumaliza elimu ya juu. Alisema yeye anajua mbinu za kitaalamu za kubadilisha hali za wananchi kutoka dimbwi la umasikini walipo sasa.

Ni ahadi iliyowakuna wananchi wa Kitope, kiasi cha kuamua kumrudisha Maalim Seif kupokea zawadi adhimu ya kupata wanachama wapya wa CUF kwa kuamini ndio chama kinachowapigania kupata maisha bora.

Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati Balozi Seif ni Makamu wa Pili nafasi inayompa pia hadhi ya kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Hawa ni viongozi wasaidizi wa Rais Dk. Shein lakini kutokana na kugubikwa na siasa za chuki, Balozi Seif amenukuliwa na mfanyabiashara aliyemuita na kumhoji kwanini wafanyabiashara wameipa CUF fedha na kununulia gari na zana za kazi kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, akisema “mimi simpendi Maalim Seif.”

Lakini Maalim Seif, mzaliwa wa Mtambwe, kisiwani Pemba mwaka 1939, mwenye shahada ya Sayansi ya Siasa, aliyosomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akionesha kuwa amezipata salamu za Balozi Seif, alijibu jukwaani kijijini Makunduchi, 29 Machi, “mimi nampenda sana Balozi.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya CUF, katika mkutano wa kesho Jumapili Kitope, wamejitokeza watu 600 watakaochukua kadi kama wanachama wapya wa chama hicho.

Wiki mbili zilizopita, Maalim Seif aliwakabidhi kadi wanachama wapya 600 wa jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini Unguja, ambako kama ilivyo kwa Kitope, ni ngome ya CCM.

Mkutano huo ambao pia utamshuhudia waziri wa zamani katika serikali ya CCM, Mansour Yussuf Himid, aliyejiunga CUF, akihutubia, unafanyika wakati Jeshi la Polisi limetoa amri ya kupiga marufuku vyama vya siasa kusafirisha makundi ya wanachama kwenda mikutanoni.

CUF wamesema hawawezi kuzuia haki ya wananchi kushiriki shughuli za siasa hasa kwa kuamini kuwazuia kwa namna yoyote ile ni kuvunja katiba ya nchi.

Polisi imetoa amri hiyo baada ya tukio la wanamaskani wa CCM kujeruhi wanachama 25 wa CUF kwa mapanga, nondo na marungu wakati wakirejea mkutano wa Makunduchi. Wanne wanaendelea kutibiwa hospitalini huku polisi wakishindwa kukamata mtu mpaka sasa.

error: Content is protected !!