Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif amdhibiti Prof. Lipumba, amshika pabaya
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif amdhibiti Prof. Lipumba, amshika pabaya

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimepiga marufuku uanzishaji wa matawi mapya na kuagiza viongozi wake ngazi ya majimbo kuwa macho na nyendo zozote za “watu fulani” kutaka kufungua matawi kwa nia ya kumfanikisha mipango ya kukihujumu chama. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Agizo hilo limetolewa kwa uongozi wa chama hicho kupitia vikao vya kamati tendaji vya matawi na majimbo nchini kote vilivyofanyika wiki mbili zilizopita, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya CUF.

Matawi yatakayoruhusiwa kufunguliwa ni yale yaliyopata idhini ya ofisi ya Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad. Agizo hili limeanza kutekelezwa Unguja na Pemba ambako inasemekana ndiko nguvu ya wasaliti wa CUF inakoelekezwa kwa sasa.

Salim Bimani, mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano na umma wa CUF, ameiambia Mwanahalisionline kwa njia ya simu kuwa chama kina haki ya kuchukua hatua mbalimbali za kujilinda dhidi ya mbinu za kukihujumu.

Viongozi wa matawi kadhaa wameithibitishia Mwanahalisionline kwamba wamepewa agizo hilo wakati wa mikutano maalum ya wajumbe wa kamati tendaji na viongozi wa ngazi ya juu wakiwemo wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama.

“Kwa hili hakuna shaka yoyote ni agizo halali tulilopewa na uongozi wa juu wa chama chetu. Tumejuilishwa rasmi kwamba ni katika kukabiliana na njama za kuzidi kukihujumu chama. Waliotueleza walisema ni agizo kutoka ofisi ya Katibu Mkuu wa chama,” mtandao huu umeelezwa.

Baadhi ya viongozi waliohojiwa na mtandao huu, wamesema agizo hilo limetokana na ukweli kwamba Profesa Ibrahim Lipumba hajachoka kutumika kukihujumu chama hicho.

“Viongozi wetu wametueleza mengi lakini kubwa ni kwamba wanajua namna ambavyo profesa Lipumba anaendelea kuvuruga chama,” ameeleza kiongozi mmoja anayetoka moja ya majimbo yaliyoko ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Profesa Lipumba, aliyevuliwa uanachama wa CUF tangu Septemba mwaka 2016, kwa tuhuma za kukisaliti chama kwa kuandaa na kutekeleza mpango wa kukihujumu chama, ikiwemo kuvunja mkutano mkuu maalum wa Ubungo Plaza wa tarehe 21 Agosti 2016, anatuhumiwa na uongozi wa juu wa chama kutaka kukiangamiza akisaidiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Msajili Francis Mutungi ambaye pia anakabiliwa na tuhuma hizo hadi kuwa mmoja wa maofisa waandamizi wa serikalini wanaoshitakiwa mahakamani na CUF, aliamua kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti halali hata baada ya kuwa alivuliwa uanachama.

Msimamo wake huo ulikuja baada ya Profesa Lipumba kushikilia ofisi kuu za CUF za Buguruni jijini Dar es Salaam licha ya kuwa alijiuzulu wadhifa huo kwa hiari yake kupitia barua ya tarehe 5 Agosti 2015 aliyomkabidhi katibu mkuu.

Miezi kumi baadaye, profesa alitangaza kutengua uamuzi huo na kutaka aruhusiwe kuingia ofisini na kuanza tena kufanya kazi za mwenyekiti.

Mkutano mkuu wa Ubungo Plaza uliridhia kujiuzulu kwake lakini ulikwama kuchagua mwenyekiti mpya. Kazi za mwenyekiti tangu hapo zimekuwa zikifanywa na Kamati ya Uongozi inayoongozwa na Julius Mtatiro.

Kwa mujibu wa taarifa za agizo la uongozi wa juu, viongozi wa matawi na majimbo wametakiwa kutoa taarifa haraka wanapoona watu wanaojitambulisha kama wanachama wa CUF wakitaka kufungua matawi popote pale nchini.

“Ukiona tu kuna bendera mpya ya chama karibu na eneo lako la uongozi au ndani ya eneo lako, piga ripoti kwa uongozi wa juu yako hadi wilaya.

“Ni jukumu la viongozi wote wa ngazi zote na jukumu mahsusi kwa walinzi wote wa chama chetu kusimamia agizo hili,” kiongozi mwingine ameiambia Mwanahalisionline akimnukuu kiongozi aliyewahutubia katika mkutano maalum wa viongozi wa matawi na majimbo ya Wilaya ya Magharibi A, mjini Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Maalim Seif amesema hatua mbalimbali zinachukuliwa na chama katika kukabiliana na mkakati mpya wa kukihujumu chama.

Maalim Seif ambaye juzi alihutubia viongozi na wanachama walioshiriki kongamano la CUF wilayani Kinondoni, alisema hatua hizo zimeidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya chama iliyokutana tarehe 25 Machi.

Zipo taarifa kuwa kundi linaloongozwa na profesa Lipumba linajitahidi kutaka kupata akidi ya wajumbe ili kuitisha watakachokiita “mkutano mkuu” ambao moja ya maazimio yanayolengwa ni kumfukuza Maalim Seif.

Mapema mwezi huu, profesa alisafiri kwa ndege kwenda kisiwani Pemba ambako aliandaliwa mkutano wa ndani kwenye ukumbi wa kiwanda cha Makonyo, eneo la Wawi, nje kidogo ya mji wa Chake Chake, na kuondoka mara baada ya mkutano huo.

Hakufanikiwa kukagua tawi lolote wala kukutana na viongozi wa wilaya kama ilivyokusudiwa awali. Walioshuhudia profesa akipokewa uwanja wa ndege wa Chake Chake, walisema ziara yake hiyo iligubikwa na ulinzi mkali wa polisi wenye sare na wasiovaa sare.

CUF inamtuhumu kiongozi mmoja katika Baraza la Mapinduzi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kushirikiana na profesa Lipumba katika mpango mpya wa kumaliza chama hicho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Askofu Wolfang Rais mpya TEC, Padri Kitima aula tena

Spread the loveBARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetambulisha safu mpya za...

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

error: Content is protected !!