July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif akaza kamba

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad ambaye anapigania haki yake ya kuongoza Zanzibar baada ya kuchaguliwa na wananchi, anataka kukutana na Rais Jakaya Kikwete “haraka leo kesho.” Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa CUF, Ismail Jussa, Maalim Seifr amemuandikia rasmi barua Rais Kikwete akitaka wakutane.

Lengo la kukutana taarifa hiyo imesema ni “kuzungumzia hali ya kisiasa ya Zanzibar kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.”

Katika taarifa hiyohiyo, imeelezwa kwamba CUF imekubali kufanya mawasiliano na wasaidizi wa Rais Kikwete ili8 kupanga utaratibu wa kumwezesha Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, kukutana na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange.

Taarifa hiyo pia imeeleza lengo la mahitaji ya kukutana na Jenerali Mwamunyange kuwa ni “kuzungumzia hali ya usalama ya Zanzibar kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.”

Kumekuwa na jitihada mbalimbali hapa za kutafuta ufumbuzi wa mkwamo ulioukabili uchaguzi mkuu kufuatia tangazo la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim Jecha la kufuta uchaguzi wakati akiwa ameshatangaza asilimia 70 ya matokeo ya kura za urais.

Alipotangaza kupitia taarifa iliyorekodiwa na kurushwa na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) hapo Oktoba 28 adhuhuri, Jecha alishatangaza hadharani matokeo ya kura za urais za majimbo 32 kati ya majimbo yote 54 ya Zanzibar.

Viongozi mbalimbali wamekuwa wakikutana na Maalim Seif pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wa CCM, kujadili njia nzuri ya kufikia muafaka. Maalim Seif amekuwa akisisitiza kuwa mgogoro unapaswa kutatuliwa kisiasa, sio kiulinzi, kwa kuzingatia Sheria na Katiba ya Zanzibar, akilenga kuelekeza kuwa Tume ya Uchaguzi ikamilishe kazi ya kuhakiki matokeo yaliyobakia na kumtangaza mshindi.

Katika jitihada hizo, leo Maalim Seif alikutana na viongozi wa dini mbili kuu nchini – Kiislam na Kristo – waliopo Zanzibar kuzungumzia mgogoro huo na umuhimu wa kupatiwa ufumbuzi kwa amani.

“Tunapenda kuwahakikishia kuwa tunachukua kila juhudi zilizomo kwenye uwezo wetu katika kuupatia ufumbuzi mgogoro na kufanya kazi na kila aliyetayari kushirikiana na sisi katika kutunza amani ya nchi yetu na kuilinda demokrasia yetu,” amesema Maalim Seif katika taarifa hiyo.

Jana alihimiza wananchi kuwa watulivu na wasichokozeke, huku akilaani mbinu za kuwatisha wananchi kupitia askari wengi waliosambazwa nchini wakizunguka na silaha nzito. Alipuuza matamko yanayotolewa na wakuu wa CCM akisema ni maoni yao yasiyoendana na hali halisi inayoendelea kupitia majadiliano.

error: Content is protected !!