April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif ailia kiapo CCM 2020

Spread the love

MAALIM Seif Sharif Hamad, mwanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo, amekula kiapo hadharani kwamba, hatolala mpaka ahakikishe kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekaa kando. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akiwa kwenye uzinduzi wa ofisi za chama hicho katika Kata ya Chanika kwenye Jimbo la Ukonga, jijini Dar es Salaam tarehe 30 Mei 2019 alisema, atafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa, analeta mabadiliko nchini.

“Hata saa nane usiku ukiniamsha, mimi nipo tayari pamoja na uzee wangu wote huu mimi sijachoka kama bado sijaleta mabadiliko kwenye nchi. Kama CCM hatujaiweka upande, bado sijaridhika.

“Nitafanya kazi usiku na mchana, naomba wenzangu wote tuungane katika hili kwa dhamira moja na tuwe na nidhamu,”amesema Maalim Seif.

Maalim Seif ambaye amelalamika kupinduliwa kwa matokeo yake ya uchaguzi katika Uchaguzi Mkuu 2015, amewaeleza wanachama waliohudhuria kwenye ufunguzi wa ofisi hizo kuwa, wakiwa viongozi ndani ya chama hiko wakubali kukabiliana na changamoto za mapambano ya kisiasa katika kuwapigania wananchi.

“…wanachama na hasa ambaye anayeomba uongozi, kila mtu anayeomba uongozi kwanza ajitathimini mwenyewe, zipo changamoto nyingi … . Ni lazima useme naungana na wenzangu kuwaletea mabadiliko katika nchi yangu ili kila mmoja kwenye nchi hii anufaike na rasilimali za nchi hii. Hili ndio lengo letu, hakuna kulala,” alisema.

Amewahimiza viongozi wajiamini katika kusimamia haki pia wawe na ushirikiano na wanachama wengine  ili kuleta umoja.

“Hakuna ambalo unaweza kulifanya pekee yako, mkishikamana mtafanya makubwa …lakini pia nidhamu, ni lazima chama chetu kiwe na nidamu ya hali ya juu kabisa” amesema Maalim Seif.

Amesema kuwa, mambo hayo (nidhamu, umoja na mshikamano) yakitendeka, CCM 2020 itajua kuwa kweli kuna upinzani. Hata hivyo amesema, ACT-Wazalendo hakiko tayari kushirikiana na vyama ambavyo vipo kimaslahi.

 “Nasema hiyo haina maana kuwa, sisi hatupo tayari kufanya kazi na wenzetu. Tupo tayari kufanya kazi na vyama vengine ambavyo vina nia ya dhati kufanya mabadiliko, sio vyama ambavyo vina tafuta maslahi,” amesema.

Amesema kuwa, CCM mwaka 2015 ilitikisika kutokana na umoja wa Ukawa akisisitiza kuwa, chama hicho tawala wanaiogopa ACT-Wazalendo hivyo wameanza kukihujumu.

“Sasa hivi hadithi nilizo nazo CCM wanakiogopa ACT-Wazalendo na mikakati yote sasa hivi ina pangwa ni jinsi gani wataihujumu ACT-Wazalendo, msiwe na wasiwasi, hawatofaulu kwasababu sisi  nia yetu ni moja, tuna nia mzuri na nchi hii na sisi tupo kwenye siasa kwa muda mrefu. Hakuna mbinu ambayo hatuijui,” aliwatoa hofu.

error: Content is protected !!