Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Maalim Seif ahofia uchaguzi mkuu kuacha majeraha
Habari za SiasaTangulizi

Maalim Seif ahofia uchaguzi mkuu kuacha majeraha

Semistocles Kaijage, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC)
Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimebainisha vikwazo kumi vitakavyosababisha uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 kutokuwa huru, haki na unaoweza kuacha majeraha kwa Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Vikwazo hivyo, vimebainishwa leo Jumatano tarehe 10 Juni 2020 na Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Maalim Seif amesema, “Tunahitaji kuwa na uchaguzi utakaowaacha Watanzania wakiwa na furaha na matumaini baada ya kutekeleza haki na wajibu wao wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi wanaowataka.”

Amesema, kwa bahati mbaya, ikiwa imesalia miezi miwili tu kuelekea kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu, mazingira ya kisiasa nchini hayatoi taswira ya uchaguzi unaoweza kuiacha nchi yetu salama.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likiwa halina umoja. Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likikosa maelewano ambayo yangefanikisha uchaguzi kufanyika kwa amani.”

“Tunakwenda kwenye uchaguzi Taifa likiwa katika mazingira mabaya na mfumo mbovu wa uendeshaji chaguzi kuliko wakati mwengine wowote wa historia yetu,” amesema katibu mkuu huyo wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF)

Maalim Seif amesema, vyombo vinavyosimamia uchaguzi, yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na vyombo vya dola kwa ujumla wake haviendeshwi katika namna itakayolivusha Taifa salama kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

“Dalili zipo wazi kama hali ya sasa itabaki kama ilivyo, bila shaka, uwezekano wa amani tunayojivunia huenda ikawa ni historia. Tunawasihi wenye mamlaka wasiifikishe nchi huko,” amesema.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Kiongozi huyo amesema, kwa kutambua wajibu wao kama chama makini cha siasa nchini humo, na kwa lengo la kusaidia kuepusha nchi isifike huko, wametoa hoja kumi zinazopaswa kufanyiwa kazi kabla ya uchaguzi huo.

Maalim Seif ametaja baadhi ya vikwazo hivyo vinavyoweza kusababisha uchaguzi huo usiwe huru kwa Tanzania bara na Zanzibar ni;

Mosi, Tume za Uchaguzi si Huru: Kwa muundo wake, Tume zetu zote mbili, kwa maana ya NEC na ZEC, zinaonekana kuwa ni Tume za Rais badala ya kuwa Tume Huru za Uchaguzi.

Mwenyekiti na Mkurugenzi wa NEC na ZEC wanateuliwa na Marais (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar) ambao pia ni Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar.

Katika ngazi ya Halmashauri, wasimamizi wa uchaguzi ni wakurugenzi wa Halmashauri ambao kwa asilimia kubwa sana ni makada wa CCM.

“Unakuwaje na Tume Huru ambayo mmoja wa makamishna wake ni Omar Ramadhani Mapuri, mtu aliyefikia kuwa katibu mwenezi Taifa wa Chama Cha Mapinduzi?

“Au kwa upande wa Zanzibar, unakuwaje na Tume Huru huku mwenyekiti wake akiwa ni mtu kama Hamid Mahmoud Hamid ambaye hajawahi kuficha hisia zake za chuki dhidi ya upinzani na dhidi ya viongozi wa upinzani Zanzibar?  Katika hali hii vipi unaweza kufikiria kuwa tunaweza kuwa na Uchaguzi huru na wa haki,” amehoji.

Pili, hujuma za wazi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika tarehe 24 Novemba 2019 ambapo, Serikali haijayafanyia kazi mapendekezo yetu ya kuufuta uchaguzi huo.

“Uchaguzi huo umesababisha kuwepo kwa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji ambao hawana uhalali wa kisheria wala wa kisiasa kwa sababu hawakuchaguliwa na wananchi,” amesema

“Kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu, ni wakati muafaka kwa mamlaka zinazohusika kutathmini kosa hili la kihistoria. Ni dhahiri hakuna maendeleo ya maana na yanayoaminika yanayoweza kupatikana kwa kusimamiwa na watu hawa kwa sababu umma hauwezi kuwaunga mkono,” amesema Maalim

Tatu, hujuma kwenye uandikishwaji wa wapiga kura Zanzibar akisema, “hivi sasa wakati tunazungumza hapa, kwa upande wa Zanzibar, ZEC wanaendelea na zoezi la uhakiki wa wapiga kura wa zamani na kuandikisha wapiga kura wapya.”

Amesema, zoezi hilo limekuwa likilalamikiwa na wananchi walio wengi akisema, “Hali hii haiwezi kutoa taaswira ya kuwa tunaweza kuwa na Uchagzi huru na wa haki.

Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma

Nne, Maalim Seif amesema, “Vyombo vya habari vya umma kujigeuza midomo ya CCM. Duniani kote vyombo vya habari vya umma hufanya kazi ya kutumikia wananchi wote kutokana na ukweli kwamba vinaendeshwa kwa fedha za walipa kodi ambao ni wananchi wote.”

“Jukumu lake kubwa huwa ni la kusimamia uwajibikaji na kusimamia demokrasia kupitia uhuru wa habari. Bahati mbaya sana kwa upande wa Tanzania na Zanzibar vyombo vyote hivi vimegeuzwa kuwa ni midomo ya CCM,” amesema

Tano, amesema, utawala wa umma kutumika kisiasa.

Amesema, pamoja na Tume ya Jaji Francis Nyalali mwaka 1992 kutaka utawala wa umma kwa maana ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri kutenganishwa na siasa na kufanya kazi za utumishi wa umma.

“Bado hakuna hatua zilizochukuliwa kulifanyia kazi pendekezo hilo. Ni miaka 28 sasa tokea kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa lakini bado nafasi za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri zimeendelea kutumiwa,” amesema.

Amesema, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao kama wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuhujumu vyama vya upinzani.

“Katika mazingira kama haya, hakuwezi kufanyika uchaguzi huru na wa haki,” amesema

Maalim Seif amesema, ili uchaguzi uwe huru na haki, “Serikali ipeleke Muswada kwa hati ya dharura kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kufanya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Katiba ya Zanzibar na Sheria za Uchaguzi ili kuzifanya Tume za Uchaguzi zote mbili, NEC na ZEC, ziwe huru.”

“Vifungu kwenye Katiba zetu na sheria za uchaguzi vinavyompa mamlaka Rais kuteua mwenyekiti, makamishna na mkurugenzi wa uchaguzi vibadilishwe, uteuzi ufanywe na chombo huru,” amesema

“Katika ngazi ya Halmashauri, uchaguzi usimamiwe na watendaji wa Tume Huru ya Uchaguzi badala ya Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wengi ni makada wa CCM. Marekebisho yanayopendekezwa pia yaruhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa mahakamani,” amesema

Amesema, “huwezi kuwa na uchaguzi huru na wa haki ambao wananchi wake kwa maelfu wanalalamika kunyimwa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.”

Maalim Seif amesema, uchagzu mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 2020 unapaswa kuonekana kuwa ni uchaguzi huru, wa haki, wa wazi na wenye kuaminika.

“Hivyo basi ni lazima ZEC na NEC ziandae mazingira rafiki yatakayoruhusu waangalizi wa Kimataifa wa muda mrefu na mfupi wanapata fursa ya kuuangalia na kuupima uchaguzi huu,” amesema.

Waandishi wa habari wakiwa katika moja ya majukumu yao ya kila siku

Amesema, wakati huo huo, Jumuiya  ya Kimataifa iwaunge mkono waangalizi wa ndani ili nao waweze kushiriki kuupima Uchaguzi huu.

Pia, Maalim Seif amesema, “vyombo vya habari vya umma vinapaswa kutoa fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa bila upendeleo wa aina yoyote. Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki.”

Kuhusu mizania ya haki, Maalim Seif amesema, “Mahakama zetu zijirekebishe na kurudisha imani ya wananchi kwamba ni vyombo vya kusimamia na kutoa haki. Majaji na Mahakimu pamoja na maofisa wengine wa Mahakama waonekane kuwa wanatenda haki na kurudisha heshima ya Mahakama zetu.”

Akihitimisha tamko lake, Maalim Seif amesema, “sisi kama Chama makini tutafanya juhudi za kuwasiliana na vyama vyengine makini vya siasa pamoja na wadau wengine kuona vipi tunaweza kufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na vikwazo hivi.”

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & TV kwa habari zaidi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaKimataifa

Mwanaye rais jela miaka miaka 6 kwa dawa za kulevya

Spread the loveMwanawe rais wa zamani wa Guinea-Bissau amehukumiwa kifungo cha miaka...

Habari za SiasaTangulizi

Mapya yaibuka wamasai waliohamishwa Ngorongoro kwenda Msomera

Spread the loveMAPYA yameibuka kuhusu zoezi la Serikali kuwahamisha kwa hiari wamasai...

Habari MchanganyikoTangulizi

Baba aomba msaada kuzika miili ya familia yake iliyofunga bila kula kuonana na Mungu

Spread the loveWAKATI Mamlaka nchini Kenya, ikiendelea kukabidhi miili ya watu waliofariki...

Habari za Siasa

Rais Samia ampongeza mpinzani aliyeshinda urais Senegal

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amempongeza mwanasiasa wa...

error: Content is protected !!