MAALIM Seif Sharif Hamad, mgombea urais Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, ameonesha wasiwasi wa kukwamishwa katika kinyang’anyiro hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).
Akizungumza katika Kongamano la Vijana wa ACT-Wazalendo tarehe 8 Septemba 2020 visiwani humo, Maalim Seif amedai, kuna baadhi ya watu wa vyama vingine wamepanga kumuwekea pingamizi katika Tume ya Uchaguzi (ZEC), ili asiteuliwe kugombea.
Amesema, anawakaribisha watu wanaotaka kumuwekea pingamizi akisema, kwamba anafahamu namna ya kupangua pingamizi zao.

“Nasikia kuna watu washapangwa na vyama vingine kuniwekea pingamizi, nawakaribisha kwa sababu kuniwekea pingamizi atakuja kutoa haja zake na ushahidi wake, na mimi naujua vilevile.
“Sioni kama kuna pingamizi yoyote kama itasimama juu yangu. Mimi nimezaliwa Mtambwe, hamjui ninyi? Ndiyo sifa ya kwanza ya mgombea urais awe Mzanzibari wa kuzaliwa sio Mzanzibari mkaribishi,” ameeleza Maalim Seif.
Kwa mujibu wa ratiba ya ZEC, zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu za kugombea urais, lilifunguliwa tarehe 26 Agosti 2020 na linatarajiwa kufungwa leo tarehe 9 Septemba 2020.
Leave a comment