January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim Seif aahidi neema Z’bar

Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad

Spread the love

MOJA ya hoja kuu alizozitoa Maalim Seif Shariff Hamad katika kuendelea kusaka urais wa Zanzibar ni kukubalika kwake kutokana na imani ambayo haijachuja aliyopewa na Wazanzibari. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Hii ni hoja muhimu inayoendana vema na kauli yake kwamba bado ana dhamira ya kuiongoza nchi kwa misingi ya uongozi mwema ambao anaamini ndio hujenga mshikamano wa wananchi na usalama na amani kwa nchi.

Kwa miaka mingi, tangu alipofukuzwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mei 1988, pamoja na wajumbe wenzake sita wa Halamshauri Kuu ya CCM kutoka Zanzibar, Maalim Seif amekuwa akirudia ahadi ya kuwa pamoja na Wazanzibari akiwa ndani au nje ya serikali.

Maalim Seif, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alichukua fomu ya chama chake Alhamisi, ya kuomba ridhaa ya kugombea urais, ikiwa ni mara yake ya tano.

Anataka urais kwa mara ya tano kwa sababu, anasema ajuavyo bado ana uwezo na afya nzuri, hana ugonjwa wowote, na zaidi, hajapata kushindwa kihalali uchaguzi mara zote nne alizogombea.

Mzaliwa wa kijiji cha Mtambwe, kisiwani Pemba tarehe 22 Oktoba 1943, Maalim Seif pamoja na chama hicho ambacho vuguvugu la kukianzisha lilianza kabla ya mageuzi ya kisiasa nchini 1992, wanaamini serikali imekuwa ikivuruga uchaguzi kwa lengo la kuing’ang’aniza CCM madarakani.

CUF imekuwa ikiamini serikali inatumia vyombo vya dola kulazimisha wakuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo yasiyo halali kwa nia ya kuisaidia CCM.

Ndio maana safari hii amesema “Sitokubali tena kunyang’anywa ushindi wakati wa uchaguzi,” akijibu risala ya kundi la wanachama waliokwenda nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji, kumkabidhi Sh. 1.5 milioni za kuchukulia fomu.

Juzi baada ya kukabidhiwa fomu katika tawi lake la Kilimahewa, mjini Zanzibar, alisema, “Nitaheshimu matokeo ya uchaguzi iwapo utakuwa huru na wa haki. Nina imani na tumejiandaa kushika madaraka tukipewa ridhaa na Wazanzibari.”

Maalim Seif alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kwa miaka minne chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, kiongozi aliyeongoza nchi kwa mafanikio makubwa akiimarisha uchumi na kuendeleza demokrasia.

Alifukuzwa CCM kwa kutuhumiwa kuchafua hali ya hewa waliposimamia hoja ya mabadiliko ya mfumo wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, ambayo miaka ya nyuma ilikuwa ndiyo hoja kuu ya mzee Aboud Jumbe Mwinyi, mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM), mjini Dodoma.

Alirudi serikalini 9 Novemba 2010, baada ya kuteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyeunda serikali ya umoja wa kitaifa ikiwa ni hatua ya utekelezaji makubaliano yaliyoasisiwa katika mkakati uliosukwa na Maalim Seif na Amani Abeid Karume aliyekuwa rais.

Maalim Seif alitangazwa kupata kura 175,338 (asilimia 49.1) dhidi ya kura 179,809 sawa na asilimia 50.1 alizotangaziwa Dk. Shein. Kura zote zilikuwa 364,924.

Maalim Seif ambaye alipata kuwa Waziri wa Elimu (1977-1980) chini ya uongozi wa mzee Jumbe, aliyemfundisha shuleni, alipata asilimia 49.8 ya kura 1995 katika uchaguzi ambao matokeo yake yalishukiwa hata na watazamaji wa kimataifa; asilimia 37 mwaka 2000 katika uchaguzi uliopingwa na watazamaji; asilimia 46 mwaka 2005 katika uchaguzi uliopingwa na watazamaji.

Huyu ni mwanasiasa ambaye akiwa nje ya CCM hata kabla ya mageuzi ya mfumo wa siasa, alikamatwa 1989 na kuwekwa jela hadi mwaka 1991. Baada ya vyama vingi kuruhusiwa 1992, alikamatwa Aprili 2000 na kufunguliwa kesi ya jinai pamoja na viongozi wengine wa CUF, wakituhumiwa kumshambulia askari polisi na kumpora bunduki. Alifutiwa mashitaka Novemba 2003.

error: Content is protected !!