October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maalim atilia neno kitambulisho cha Mzanzibari

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad amepokea kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi huku akitoa neno kwamba “wala hakuna sababu ya msingi ya kutolewa kitambulisho kipya.” Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Maalim ambaye amekabidhiwa kitambulisho kwa hadhi yake ya kuwa makamu wa kwanza wa rais mstaafu wa Zanzibar, alipokea kitambulisho chake nyumbani kwake Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar akikabidhiwa na afisa aitwaye Khatib Bakari kutoka Wakala wa Usajili wa Kitambulisho na Matukio ya Kijamii.

Hafla hiyo inafanyika miezi mitano tangu Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akabidhiwe kitambulisho chake na ikiwa ni karibu miaka miwili tangu pale wananchi walipojitokeza vituoni kuandikishwa upya, hatua iliyoelezwa kuwa ni ya kuimarisha taarifa zilizotunzwa kwenye kitambulisho cha awali kilichotolewa kuanzia mwaka 2005.

Aidha, Wakala wa Usajili wa Kitambulisho anamkabidhi Maalim Seif kitambulisho chake huku kukiwa na urasimu wa usiomithilika wa kupata kitambulisho hicho mwananchi mwezi mzima sasa tangu kilipoanza kutolewa kwa kuanzia Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa.Kaskazini Pemba.

Kitambulisho tangu wiki iliyopita kimeanza kutolewa kwa mikoa mitatu ya Unguja, ikianzia kisiwa cha Tumbatu, ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa sasa utoaji unaendelea kwa wilaya mbili za Magharib A na.Mgharib B kabla ya kuingia Wilaya ya Mjini hivyo kukamilisha utoaji katika mkoa wenye zaidi ya asilimia 45 ya wananchi wa Zanzibar.

Ukweli huo wa urasimu katika kupatikana kwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ambacho ni haki ya kisheria, ndio uliomsukuma Maalim Seif kutoa nasaha kwa Wakala wa Usajili na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuonya kuwa kitambulisho kinaweza kuzusha balaa pale wananchi watakapochoka kuvumilia kunyanyaswa.

Maalim Seif amesema ni jambo la aibu na la kuchochea hasira za wananchi kuwaita wasajiliwe kwa ajili ya kupatiwa kitambulisho na mwishoni ukawasumbua kukipata.

“Inasikitisha kuona kwamba Serikali imetoa kitambulisho lakini papo hapo ikaweka urasimu katika kuwapa wenyewe wananchi… na sheria inakataza afisa yeyote wa serikali kumzuilia mwananchi kitambulisho chake,” alisema mbele ya waandishi wa habari nyumbani kwake.

Amesema katika hali ya kawaida kitambulisho hicho si suala la kisiasa lakini inashangaza wakati viongozi wanajua kuwa kitambulisho kina matumizi mengi ya mahangaiko ya maisha ya watu, “pamewekwa urasimu mkubwa hata kukipata.”

“Ni mkakati maalum wa kisiasa wa CCM kupunguza wapiga kura hasa wale wanaoonekana ni wafuasi wa vyama vya upinzani. Pemba zaidi ya watu 50,000 hawakupatiwa vitambulisho vyao. Ni mkakati wenye nia ovu dhidi ya demokrasia na unakusudia kuvuruga amani ya nchi. Watu wanajengwa hasira makusudi.”

Alitoa nasaha kwa uongozi wa Wakala wa.Usajili kujitenga na kuwanyanyasa wananchi waliowaandikisha. Idara hizi ni za umma kwa lengo la kuwahudumia wananchi na sio kwa malengo ya kisiasa.

Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kinahitajika pale mwananchi anapotaka leseni ya biashara, leseni ya gari, kupeleka mtoto skuli ikiwemo anapoingia darsa la kufanya mtihani wa kitaifa, kusajili ardhi, mashirika na asasi za kiraia kuomba pasipoti.

Lakini mwwnendo wa utoaji wa kitambulisho kwa mazoea umekuwa ukichukuliwa kama silaha ya kisiasa kwa kuwa Mtanzania ambaye ni Mzanzibari hawezi kuandikishwa kuwa mpigakura mpaka awe na kitambulisho hicho.

Dk. Shein ambaye anamaliza muhula wa pili wa kuwa rais na kutatajiwa kustaafu Oktoba mwaka huu, alipata kusema kwa kuwa ZAN ID serikali itaweka na kuhifadhi kumbukumbu za matukio ya watu wote katika Daftari la Usajili na Utambuzi.

Alisema matumizi ya kitambulisho hicho yataisaida Serikali, taasisi na watu binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zenye mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.

Akaongeza kuwa kuwepo kwa mfumo huo wa matumizi ya kitambulisho kipya kutaisadia serikali katika kuwatambuwa watu wanaostahiki kupata haki za msingi kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.

“Mfumo mpya utawezesha kumtambua mtu anaestahiki kupata haki kama vile malipo ya pensheni, haki za matibabu, kujiunga na masomo na nyenginezo,” alisema mara baada ya kukabidhiwa kitambulisho chake Oktoba mwaka jana.

Alihimiza kila mwananchi kutembea na kitambulisho chake mahala popote ndani ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usajili na matukio ya kijamii Zanzibar, Dk. Hussein Khamis Shaaban alisema idara yake itaendelea kusajili na kuwapatia vitambulisho wananchi wote wenye sifa za kisheria. Sheria inayohusu kitambulisho hicho ni ya mwaka 2005.

Alisema mfumo wa vitambulisho vya kielektroniki ni ufunguo katika kufikia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kudumisha ulinzi na usalama katika nchi.

Zanzibar alisema, inakabiliwa na changamoto kubwa ya uingiaji holela wa wageni kutoka nje, hivyo kuwepo kwa vitambulisho hivyo ni muhimu kwani kutawezesha kuwatambuwa wageni hao.
Ends.

error: Content is protected !!