May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Maajabu kaburi la Maalim Seif

Spread the love

 

BAADHI ya watu wanaokwenda kuzuru kaburi la Maalim Seif Sharif Hamad (77), aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, wanadaiwa kuchota mchanga wa kaburi hilo na kutokomea nao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Maalim Seif aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alizikwa kijijini kwao Mtambwe, Mkoa wa Kaskazini Pemba tarehe 18 Februari 2021.

Taarifa za kuchotwa mchanga wa kaburi la Maalim Seif, zimetolewa jana Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 na kiongozi wa familia ya mwanasiasa huyo, Seif Ali Seif baada ya viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba walipotembelea kaburi hilo.

Seif amedai, baadhi ya watu wanaotembelea kaburi hilo kwa lengo la kufanya dua, hubeba mchanga huo na kuondoka nao, wakidai kwamba unanukia harufu nzuri ya marashi.

“Wale watu waliondoka nao kwa sababu walisema ule mchanga una harufu nzuri, baadhi ya watu wengine walikuja wakaunusa wakasema unanukia mafuta mazuri. Wengine wanasema wanukia miski, sasa nikawauliza vipi unanukia? kweli wakasema unanukia kweli,” amesema Seif.

Seif amesema, mara kadhaa amekuwa akiwakataza watu hao kuchukua mchanga huo, ili wasije wakautumia vibaya katika imani za kishirikina.

“Wakishaunusa wegine wanaondoka nao, huwa nawaambia uacheni hapo hapo, msiuchukue mkafanyia mambo ya kishiriina,” amesema Seif.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amepiga marufuku watu wanaodhuru kaburi hilo, kubeba mchanga wake na kuondoka nao.

“Endelea kuwazuia sababu binadamu hatuwezi pata ukomo wake, hatujafahamu huu mchanga wanauchukua kwa ajili gani. Na hawa watu wanaochukua huu mchanga, wanakwenda kuufanyia nini.

Kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, nilitolee tamko hili kuhakikisha waje hapa kama wataka, ila mchanga wasiuchukue,” ameagiza Salama.

Maalim Seif Sharrif Hamad, Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, ACP Juma Sadi Khamis amesema, jeshi hilo litawakamata watu watakaobeba mchanga wa kaburi hilo.

“Watu wanaokuja kumuomebea dua, wanachukua mchanga si jambo zuri, sababu ni katika mambo hayapendezi, watu kuruhusiwa kusoma dua ni jambo la kawaida.

“Lakini si mtu akichukua mchanga, tukipata taarifa hizo atakuwa anakosea si jambo jema, mtu akifanya hivyo, tutamhesabu mkosa,” ameonya ACP Khamis.

Naye kiongozi wa dini mkoani humo, Sheikh Omari Hamad, ametoa wito kwa wananchi hao kuachana na vitendo hivyo.

“Tunajua kwamba Maalim Seif tunampenda sana, lakini kitendo cha kuchukua mchanga hatujui nini unaenda kuufanyia, wengine watauchukua kwa nia mbaya.”
“Mahaba yakipindukia, tutamfanya kuonekana hajafanya jambo kubwa dunia. Naomba mchanga tuuache,” amesema Sheikh Hamad.

error: Content is protected !!