Friday , 19 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Maadhimisho fistula 2021, CCBRT yatoa wito
Afya

Maadhimisho fistula 2021, CCBRT yatoa wito

Spread the love

 

IKIWA zimebaki siku mbili kuelekea maadhimisho ya kutokomeza Fistula ya Uzazi, bado takwimu zinaonyesha, idadi ya wanawake wenye tatizo hilo imekuwa ikiongezeka. Anaripoti Jemima Samwel, DMC…(endelea).

Maadhimisho hayo yanayofanyika kila mwaka, kwa mwaka 2021 yana kauli mbiu ni ‘Haki za Wanawake ni haki za binadamu, tokomeza fistula sasa” na yatafanyika tarehe 23 Mei 2021, katika Hospitali ya CCBRT, mkoani Dar es Salaam.

Akizungumzana na waandishi wa habari, leo Ijumaa, tarehe 21 Mei 2021, Mkurugenzi Mtendaji wa CCBRT, Brend Msangi amesema, mahitaji ya wanawake na wasichana walio katika hatari ya kupata fistula na wale wanaoishi na fistula, hayapaswi kupuuzwa.

Amesmea, ndio maana Serikali ya Tanzania na wadau wake, imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma na kutibu akina mama wenye matatizo hayo.

“Tangu mwaka 2003, tulipoanza kutibu fistula ya uzazi kama nchi, zaidi ya akina mama 17,000 wamepatiwa matibabu ya fistula, na CCBRT kwa kushirikiana na hospitali washirika wamechangia matibabu haya wa zaidi ya asilimia 50,” amesema

“Hata hivyo, idadi hii haitoshi kwa kuwa bado wakina mama wapya wanaendelea kuibuliwa wakiwa na fistula na maelfu hubaki majumbani kila mwaka bila kupata matibabu,” amesema Msangi.

Amesema, milipuko ya magonjwa na kutokuwepo kwa usawa katika nyanja za kijamii, kiuchumi ,ulemavu na kukosekana kwa usawa kijiografia huchangia kwa kiasi kikubwa wanawake na wasichana kutopata huduma za kuzuia na kupata matibabu ya fistula.

“Misaada bado inahitajika ili kuhakikisha gharama za matibabu zisiwe kikwazo cha akina mama kupata matibabu hivyo, tunatoa wito kwa wadau haswa Watanzania kujitokeza kuwasaidia mama zetu.

“Sisi kama CCBRT tunawashukuru sana washirika wetu wote ndani na nje ya nchi kwa kutuunga mkono kuwafikia wanawake hawa haswa wa mikoani,” amesema.

Hata hivyo, Daktari Bingwa wa upasuaji wa fistula wa CCBRT, Dk. James Chapa amesema, fistula ya uzazi ni moja ya majeraha mabaya yanamtokea mwanamke anayejifungua kwa uzazi pingamizi na kukosa msaada wa haraka.

Dk. Chapa amesema, majeraha haya humsababishia tundu lisilo la kawaida kati ya kizazi na njia ya haja ndogo au haja kubwa na kumuacha mwanamke akivujwa na haja kubwa au ndogo bila kuhisi amebanwa na haja kutokuwa na uwezo wa kujizuia.

“Hali hii humsababishia mwanamke huyu matatizo kisaikolojia na kuwa mnyonge na wakati mwingine, kutengwa na jamii hivyo, kuishi katika upweke na umaskini wa kutupwa.

“Tatizo hili linatibika, kuzuilika na kutokea kwake ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kwa bahati mbaya janga la sasa la ugonjwa COVID-19 nalo linaweza kuathiri hatua za kinga dhidi ya fistula katika nchi zinazoendelea ambapo fistula ya uzazi bado ipo ikiwemo Tanzania,” amesema Dk. Chapa

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

AfyaHabari za Siasa

Serikali yasaka watumishi afya ngazi ya jamii 8,900

Spread the loveSERIKALI imeanza utekelezaji wa mpango jumuishi wa wahudumu wa afya...

AfyaHabari za SiasaTangulizi

Bima ya afya kwa wote kuanza Aprili, wajane kicheko

Spread the loveSHERIA ya Bima ya Afya kwa Wote, inatarajiwa kuanza kutumika...

AfyaHabari Mchanganyiko

Marekani kuipa Tanzania bilioni 980 kudhibiti VVU, UKIMWI

Spread the loveSERIKALI ya Tanzania inatarajiwa kupewa msaada wa fedha kiasi cha...

AfyaHabari Mchanganyiko

Wanavijiji wajenga zahanati kukwepa umbali mrefu kupata huduma

Spread the loveWANAVIJIJI wa Kata ya  Musanja Jimbo la Musoma Vijijini, mkoani...

error: Content is protected !!