June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ma-RC kuwatafutia suluhu wakulima na wafugaji

Spread the love

JORDAN Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ametaka kufanyika kwa kikao cha pamoja kati yake na Dk. Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Manyara ili kujadili ufumbuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji wa mikoa hiyo, anaandika Dany Tibason.

Rugimbana ametoa wito huo wakati akizungumza na Bendera muda mfupi baada ya kukabidhiana mwenge wa Uhuru, mpakani mwa Dodoma na Manyara.

“Kutokana na maandalizi ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, kuna kila sababu ya kuwa na vikao vya pamoja kwaajili ya kupambana na changamoto zinazoweza kujitokeza. Manyara ni mkoa jirani hivyo, tusingependa kuona migogoro ya ardhi ikijitokeza kati ya wakulima na wafugaji,” amesema.

Kwa upande wake Dk. Bendera, amesema uwepo wa vikao vya pamoja katika mikoa hiyo ni jambo jema, litakalosaidia kuboresha mahusiano baina ya wakulima na wafugaji hususani katika Wilaya za Kondoa na Kiteto ambapo mapigano baina yao yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara.

“Serikali haiko tayari kuona watu wakiendelea kuuana na kuumizana kutokana na mapigano ambayo yanatokana na ugomvi wa ardhi. Jamii inatakiwa kujijengea utamaduni wa kupendana na kuhakikisha wanakaa meza moja kwa mazungumzo badala ya kupigana,” amesema.

Dodoma na Manyara ni mikoa jirani inayopakana, ambapo jamii za wakulima na wafugaji wamekuwa na mivutano ya kugombea ardhi mara kwa mara. Mivutano hiyo husababisha mapigano na vifo vya watu pamoja na wanyama.

 

error: Content is protected !!