October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ma- RC, DC na RAS waapishwa Ikulu

Rais John Magufuli akimuapisha Mariam Perla Mbaga kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amewaapisha wakuu wa mikoa (RC) na Katibu Tawala (RAS) aliowateua wakiwemo wakuu wa mikoa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia, Rais Magufuli ameshuhudia viapo kwa wakuu wa wilaya mbalimbali nchini humo vilivyofanywa na wakuu wa mikoa wa maeneo husika.

Hafla hiyo ya viapo, imefanyika leo Jumatatu tarehe 6 Julai 2020, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Wa kwanza kuapishwa amekuwa; Thobias Andengenye, aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Andengenye amechukua nafasi ya Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga ambaye amestaafu.

Baadaye akafuata, Dk. Philemon Sengati kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Dk. Sengati alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza ambaye amechukua nafasi Aggrey Mwanri ‘mzee wa sukuka ndani’ aliyestaafu.

 

Pia, Rais Magufuli amemwapisha Mariam Perla Mmbaga kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu (RAS).

Mariam alikuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Mariam amechukua nafasi ya Jumanne Sagini.

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kuwaapisha, imefuata wakuu wa mikoa kuwaapisha wakuu wa wilaya.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare amemwapisha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Ismail Twahir Mlawa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Mlawa alikuwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Morogoro ambaye amechukua nafasi ya James Mugendi Ihunyo ambaye amestaafu.

 

Pili, Sanare amemwapisha Albinus Mgonya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero (DC) Mkoa wa Morogoro.

Kabla ya uteuzi huo, Mgonya alikuwa Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Rukwa na anachukua nafasi ya Mohamed Mussa Utaly.

Tatu, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amemwapisha Kanali Mathias Kahabi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera. Kanali Kahabi anachukua nafasi ya Saada Malunde ambaye amestaafu.

Nne, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta amemwapisha Abbas Kayanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mkoa wa  Arusha.

Kabla ya uteuzi huo, Kayanda alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu na anachukua nafasi ya Theresia Jonathan Mahongo ambaye amestaafu.

Tano, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amemwapisha Mhandisi Martine Ntemo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

 

Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Ntemo alikuwa Mhandisi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na anachukua nafasi ya Asumpter Nshunju Mshama ambaye amestaafu.

Sita, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amemwapisha, Toba Alnason Nguvila kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni

Kabla ya uteuzi huo, Nguvila alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Longido Mkoani Arusha ambaye amechukua nafasi ya Godwin Gondwe ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam. Godwin Gondwe anachukua nafasi ya Felix Jackson Lyaniva ambaye amestaafu.

Saba, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemwapisha Lazaro Jacob Twange kuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara. Bwana Twange amechukua nafasi ya Elizabeth Simon Kitundu ambaye amestaafu.

Nane, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amemwapisha Wilson Samwel Shimo kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Mkoa wa Geita. Kabla ya uteuzi huo, Shimo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida.

Tisa, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amemwapisha Jamila Yusuf kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda.

Jamila alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma na anachukua nafasi ya Lilian Charles Matinga ambaye amestaafu.

 

Kumi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amemwapisha, Salum Kali kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza.

Kabla ya uteuzi huo, Kali alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza ambaye amechukua nafasi ya Dk. Philemon Sengati ambaye ameapishwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Baada ya viapo hivyo kumalizika, wakuu hao wa mikoa na wilaya, waliungana na wakurugenzi walioteuliwa wa halmashauri kula kiapo cha maadili ya viongozi wa umma.

Wakurugenzi hao ni; Mosi, Duncan Golden Thebas, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara.

Thebas alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa jijini Dodoma na anachukua nafasi ya Mussa Chimae.

Pili, Mwailafu Thomas Edwin, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara.

Edwin alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoa wa  Singida na anachukua nafasi ya Oscar Antony Ng’itu.

Tatu, Erica Epaphras Yegella, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mkoa wa Mtwara.

Yegella alikuwa Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Mbeya ambaye amechukua nafasi ya Omari Juma Kipanga.

Nne, Hassan Njama Hassan, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro.

Hassan alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji wa Mtwara Mkoa wa Mtwara na anachukua nafasi ya Florent Kayombo.

Tano, Kanyala Malima Mahinda, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mkoa wa Morogoro.

Kanyala Malima Mahinda alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani na anachukua nafasi ya Francis Ndulane.

Sita, Anastazia Tutuba, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro.

Tutuba alikuwa Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Mkoa wa  Arusha na anachukua nafasi ya Anna-Claire Shija.

Saba, Saad Mutambule kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Mkoa wa  Arusha.

Mutambule alikuwa Afisa Mipango wa Jiji la Mbeya mkoani Mbeya na anachukua nafasi ya Alvera Ndabagoye ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Nane, Elias Amede Ng’wanidako, Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mbeya Mkoa wa Mbeya.

Ng’wanidako alikuwa Mweka Hazina wa Jiji la Mbeya na anachukua nafasi ya James Kasusura ambaye amestaafu.

Godwin Gongwe, Mkuu mpya wa wilaya ya Temeke, akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya amemhakikishia Rais Magufuli kwamba atakwenda kufanya vyema pasina kumwangusha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa amesema, kila mmoja kwa nafasi yake ili kuchochea maendeleo ili kutimiza adhima ya Serikali ya awamu ya tano.

Ndikolo ametoa wito kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wateule, kufanya kazi kwa kumsaidia Rais Magufuli hususan kutatua changamoto na kero za wananchi zinazowakabili.

Amesema, haipendezi Rais Magufuli anapofanya ziara katika maeneo mbalimbali, anakutana na kero na changamoto za wananchi ambazo zingeweza kutatuliwa na wao lakini haifanyiki.

Mkuu huyo wa mkoa amesema, ni wakati wa kila mmoja aliyepewa dhamana na Rais Magufuli aweze kumsaidia kwani baadhi ya kero na changamoto ziko ngazi ya kijiji lakini kusubirio hadi mkuu wa nchi aje kuzitatua haipendezi.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online na MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!