MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewakabidhi majukumu matano wakuu wa wilaya za mkoa huo, walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 19 Juni 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Makalla amekabidhi majukumu hayo, leo Jumatatu tarehe 21 Juni 2021, wakati akiwaapisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kherry James na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Almasi Nyangasa, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Jukumu la kwanza ni ukusanyaji mapato, ambapo amewataka wakuu wa wilaya hao kusiammia ukusanyaji na matumizi ya mapato.
“Neno mkuu nimegawanya kwa vipaumbele, M ya kwanza ni mapato. Mkasimamie mapato, kila ukiniambia mkuu salama, kumbuka M ya kwanza ni mapato,”
“Ili Serikali iweze kuhudumia wananchi wake na ikafanya maendeleo lazima tuwe na mapato, mkasimamie mapato katika wilaya zenu, mkadhibiti mapato,” amesema Makalla.
Makalla ametaja jukumu la pili kuwa ni kutatua kero za wananchi wa maeneo yao.
“Jukumu lingine mkasikilize kero za wananchi, unaponiambia mkuu maana yake mkawe karibu na wananchi. Msikilize kero za wananchi, watu wetu wana changamoto kuanzia chini, kwenye mtaa hadi halmashauri, wote tukasikilize kero za wananchi,” amesema Makalla.
Viongozi hao wapya, wameelezwa kwamba jukumu lao la tatu ni ulinzi na usalama, ambapo Makalla amewataka wakaunde mikakati madhubuti ya kupambana na uhalifu hasa wizi ulioibuka hivi karibuni wa vifaa vya magari.

“Nyie mnaenda kuwa wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, lazima tuhakikishe wananchi wetu wanakuwa salama katika maeneo yao. Tupambane na uhalifu, sasa hivi kuna wimbi la wizi wa vifaa vya magari, mtu unaamka asubuhi gari halipo kila kitu kinakokotolewa,” amesema Makalla.
Makalla ametaja jukumu la nne kuwa ni usafi “nataka Dar es Salaam iwe safi, weka mikakati katika wilaya yako kusimamia usafi, Jiji la Dar es Salaam lazima liendelee kuwa taswria ya Tanzania.”
Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, ametaja jukumu la mwisho kuwa ni, usimamizi wa miradi ya maendeleo.
“Jukumu lingine la mwisho, usimamizi wa miradi ya maendeleo, tukasimamie kila mradi. Uujue mradi uliopo katika eneo lako, uufuatilie na utekelezaji wake kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema Makalla.
Ahsante Mheshimiwa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi