July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

M/kiti CCM awapa somo wapinzani madai Katiba mpya

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza, Dk. Anthony Diallo, amewataka wanasiasa wa vyama vya upinzani Tanzania, wadai mifumo bora ya uendeshaji nchi, badala ya katiba mpya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza…(endelea).

Dk. Diallo alitoa wito huo jana tarehe 9 Julai 2021, akizungumza katika kipindi cha Ajenda, kinachorushwa na kituo chake cha televisheni cha Star Tv, jijini Mwanza.

Mwenyekiti huyo wa CCM Mwanza, alisema uwepo wa katiba nzuri hauna maana kama mifumo ya uendeshaji nchi sio imara.

 

“Nchi za Ki-Afrika zinafanya makosa sana kuona kama katiba ndiyo tatizo, tatizo liko kwa watu. Mnafanya makosa mnaweka rais ambaye atakuja kuvuruga hiyo katiba, kwani katiba ya leo inaruhusu mtu anawekwa magereza bila kupelekwa mahakamani? Lakini limefanyika,” alisema Dk. Diallo.

DK. Diallo alidai kuwa, hata kama nchi ikiwa na Katiba nzuri, kisha wananchi wakafanya makosa kuchagua kiongozi asiye na maadili, itavunjwa.

“Tatizo letu ni mtu wala sio katiba, kwa hiyo hata tukitengeneza nzuri namna gani, tukaweka rais ambaye hataki kuifuata atavuruga tu. Taasisi huwa hazijengwi na wanasiasa, mihimili ya nchi inajengwa na mifumo,” alisema Dk. Diallo.

Hata hivyo, Dk. Diallo alishauri kama mchakato wa upatikanaji katiba mpya utaanza, usisimamiwe na vyama vya siasa, ili kuondoa upendeleo.

“Kuna tatizo watu hawajui, katiba maana yake ni nini haswa, kwa sababu unapoingiza chama kuanza kuidai, halafu unahusisha wao kwenye kuitunga, huo mchakato hauwezi kwenda mbali, itafika mahala mtashindwana,” alisema Dk. Diallo.

Dk. Diallo alisema mchakato wa marekebisho ya katiba ulioanza 2011 chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, ulikwama kwa sababu ya kuongozwa na wanasiasa.

“Masuala ya katiba wanasiasa tunafanya makosa kujiingiza , ukijiingiza mwanasiasa kwenye katiba itakuwa na upendeleo tu. Utataka kujipendelea, wanasiasa hawatakiwi kuingia mule, ndiyo kosa tulilofanya,” alisema Dk. Diallo.

Dk. Diallo aliongeza “Tuwe tunalilia mifumo thabiti ya nchi, katiba sawa lakini zisitengenezwe na wanasiasa, tatizo lilianzia hapo misimamo ikashindikana kila mmoja na lwake.”

Mchakato wa upatikanaji katiba mpya, ulisimama 2015 ukiwa katika hatua ya wananchi kupiga kura ya maoni, ya kupitisha rasimu ya katiba iliyokuwa inapendekezwa na lililokuwa Bunge la Katiba.

Kura ya maoni ilisitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutokana na uandikishaji daftari la wapiga kura kutokamilika.

Mchakato huo wa marekebisho ya katiba ulianza rasmi 2011 , baada ya Serikali kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013, iliyotungwa 2013.

Kufuatia kusimama kwa mchakato huo, vyama vya siasa na baadhi ya Asasi za Kiraia (AZAKI), wameanzisha vuguvugu la kuitaka Serikali iufufue kwa ajili ya kupata katiba mpya.

error: Content is protected !!