June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lyimo ahoji fedha za ukarabati

Majengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Spread the love

MBUNGE wa Viti Maalum, Suzan Lyimo (Chadema), ameihoji serikali na kuitaka ieleze ni kwanini fedha inayotengwa kwa ajili ya ukarabati wa vyuo vya zamani haifiki kwa wakati.

Katika swali lake bungeni leo, ameuliza kuwa, vyuo vikuu hasa vya zamani vimekuwa vikilalamika kutotengewa fedha za ukarabati wa majengo hali inayohatarisha maisha ya wanafunzi na kuhoji ni kwanini fedha inayotengwa kwa ajili hiyo haifiki kwa wakati.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga kwa niaba ya Waziri wa Elimu Mafunzo ya Ufundi, amesema kuwa serikali imekuwa ikitenga na kupeleka fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu vyuoni kulingana na upatikanaji wa fedha kila mwaka.

Amesema mwaka 2010/11, fedha zilizopelekwa vyuoni ni Sh. 29.4 bilioni, mwaka 2011/12 Sh.17.1 bilioni, mwaka 2012/13 Sh. 18.7 bilioni na mwaka 2013/14 zilizopelekwa vyuoni ni Sh. 7.7 bilioni.

Ameongeza kuwa, katika mwaka wa fedha 2014/15 hadi kufikia Aprili 15, 2015  jumla ya Sh. 3.9 bilionizilipelekwa vyuoni.

Kwa mujibu wa Makongoro, sambamba na kupeleka fedha za maendeleo vyuoni, serikali kupitia mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika kipindi cha mwaka 2008/2009 hadi mwaka 2013/2014, imegharamia ujenzi wa majengo mapya 25 na kufanya ukarabati wa majengo yaliyokuwepo katika vyuo vikuu.

Alivitaja vyuo vikuu hivyo kuwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Amesema kuwa mradi huo umewezesha kupatikana kwa nafasi za ofisi za wahadhiri, wakufunzi, wakutubi na wataalamu wa maabara 1,794 na vyumba vya mhadhara vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 47,622 vimepatikana katika taasisi hizo tajwa.

error: Content is protected !!