January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lwenge: Ondoeni magari yanayopata ajali

Mabaki ya gari lililopata ajali ya barabarani

Spread the love

WAMILIKI wa magari wametakiwa kufuata sheria ya kuyaondoa barabarani magari yao yanayopata ajali ndani ya saa sita. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Gerson Lwenge wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Al-Shaymaa Kwegyir (CCM).

Katika swali lake, Kwegyir alitaka Serikali kutunga sheria ya kuwawajibisha wamiliki wa magari yanayopata ajali kulipa gharama za kunyanyua magari yao badala ya kuwatumia askari wa usalama barabarani.

Mbunge huyo pia alitaka kujua kama ipo bei elekezi inayotumika kuwaongoza wamiliki wa winchi kwa kazi ya unyanyuaji wa magari yanayopata ajali.

Lwenge amesema gari linapopta ajali ni wajibu wa mmiliki kuhakikisha anaondoa gari lake mapema iwezekanavyo ili kutokuwa na kizuizi cha kufunga barabara.

Amesema Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2007 inaeleza kuwa gari lolote linaloharibika barabarani linatakiwa kuondolewa na mmiliki.

“Hakuna bei elekezi ya kuwaongoza wamiliki wa winchi kwa kazi ya unyanyuaji wa magari yaliyopata ajali bali kinachofanyika ni maelewano kati ya mwenye winchi na mmliki wa gari lililopata ajali,” alisema.

Amesema kwa mujibu wa sheria hiyo, inaeleza wazi kuwa endapo wamiliki wa magari yanayopata ajali barabarani watachelewa kuita winchi la kuliondoa gari ndani ya barabara, mamlaka ya barabara italiondoa na wamiliki wanawajibika kulipa gharama zilizotumika.

Kwa mujibu wa Lwenge, mbali na kulipa gharama hizo pia mmiliki atatakiwa kulipa faini zitakazoamuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Barabara.

error: Content is protected !!